The House of Favourite Newspapers

Aweso aagiza mradi wa Maji Nzuguni ukamilike ndani ya siku 30 – Video

0

Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso(MB) akizungumza na watendaji wa Wizara ya Maji na Viongozi wa Mkoa wa Dodoma amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph kukamilisha Utekelezaji wa Mradi wa Maji Nzuguni ndani ya Mwezi mmoja na pia ndani wa siku saba (7) wanachi waanze kupata huduma hiyo hatua kwa hatua wakati hatua za ukamilishaji wake zinaendelea ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Pia ameongeza kuwa wakandarasi wote waongeze bidii na kufanya kazi usiku na mchana na kuongeza kasi ili lengo na dhamira hii viweze kutimia.

Katika hatua nyingine; Waziri Aweso ameeleza kwamba Mradi anaifahamu vema Changamoto ya Maji kwa katika Jiji la Dodoma hususani baada ya Makao Makuu ya Serikali kuhamia mahapa hapa na kusababisha ongezeko kubwa la wakazi na kueleza kuwa anaipongeza kwa dhati Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma kwa Juhudi ambazo inazifanya kuhakikisha Dodoma inakuwa Salama pamoja na uhaba wa Maji uliopo na kuipongeza kwa kazi iliofanyika hadi sasa katika utekelezaji wa Mradi huu wa mipango ya muda mfupi.

Akizungumzia hilo Mhe Aweso amesema;- “Tunazo Juhudi za Muda Mfupi za Mradi wa Maji wa Nzuguni AWAMU YA KWANZA. Tunatekeleza mradi wa 4.3bn na umefikia asilimia 93 ya utekelezaji. Kazi iliyobakia ni ndogo na inakamilishwa ndani ya kipindi kifupi cha mwezi mzima. Maelekezo yangu ni DUWASA ianze kuhudumia wananchi ndani ya siku 7 zijazo kwa asilimia hizo zilizofikiwa wakati ikikamilisha hatua za mwisho.”

Mradi wa maji Nzuguni utaongeza asilimia 11.7 na utahudumia wakazi zaidi ya 75,000 katika maeneo ya Nzuguni yote, Kisasa Nyumba 300, Ilazo na Swaswa.

Aidha Aweso ameeleza kwamba DUWASA imeanza utekelezaji wa mradi wa Uchimbaji wa Visima vingine vitano (5) kwa AWAMU YA PILI katika eneo hilohilo la Nzuguni. Kazi hiyo inalenga kuongeza maji kwa asilimia zisizopungua 15 na kuhimiza kazi hiyo nayo iendelee kwa haraka.

Pia, kazi ya kuchimba kisima cha mita 300 kwa mara ya kwanza katika Jiji la Dodoma kama ilivyoelekezwa na wataalamu kuwa kuna uwezekano wa kupata maji mengi zaidi ya kumaliza tatizo la maji Dodoma ianze mara moja na ndani ya miezi miwili tupate majibu ya kazi hiyo.

Mwisho Waziri Aweso amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan itaendelea kwa kuwajali wananchi wa jiji la Dodoma pamoja na uwepo wa mipango ya muda wa kati yaani Ujenzi wa Bwawa la Farkwa na mpango mkubwa wa Muda mrefu wa kutumia chanzo cha Ziwa Victoria bado mipango ya muda mfupi kama hii itaendelea kwa kasi ili kunusuru hali halisi ya changamoto ya Maji Jijini Dodoma.

Leave A Reply