The House of Favourite Newspapers

Mjane wa Mrema Aonja Urithi wa Mali, Utata wa Ndoa Wamalizwa

0

Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke kimetoa uamuzi juu ya urithi wa mali za marehemu Augustino Lyatonga Mrema ambapo imemtaja mjane wa Mremba Doris kuwa mnufaika wa mirathi hiyo.

Uamuzi huo umetolewa tarehe Oktoba 20, 2023 na Jaji Augustine Rwizile ambapo ameeleza kuwa Peter Mrema ndiye msimamizi pekee wa mali zilizoachwa na marehemu Mrema huku mjane wake akikataliwa kuwa msimamizi wa mali hizo.

Katika uamuzi huo umewaorodhesha watu tisa watakaonufaika ambao ni pamoja na Doris Agness Augustin Mkandala (45) ambaye ndiye mjane wa Mrema, Elizabeth Augustino Mrema (52), Mary Augustino Mrema (48), Cresencia Augustino Mrema (45), Elizabeth Augustino Mrema (43), Michael Augustino Mrema (40), Edward Augustino Mrema (38), Peter Augustino Mrema (37), na Godlove Augustino Mrema (18).

UTATA WA NDOA WAMALIZWA

Hukumu hiyo imetolewa baada ya mtoto wa Mrema, Peter Augustino Mrema kuwasilisha ombi katika mahakama hiyo la kutaka mjane wa marehemu, Doris aondolewe katika usimamizi wa mali na wala asihusishwe kwa kuwa hakuwa mke halali wa marehemu baba yao.

Pia Peter alitaka baadhi ya watoto wa marehemu wasihusishwe katika ugawaji wa mali hizo jambo ambalo mahakama pia imelipinga.

Hata hivyo, uamuzi huo umedai kuwa ndoa aliyofunga Mrema na Dorris tarehe 24 Machi 2022 katika Kanisa Katoliki Parokia Uomboni, Marangu mkoani Kilimanjaro, ni ndoa halali.

Mahakama hiyo imedai kuwa licha ya Doris kukiri kuwahi kufunga ndoa kabla ya kufunga ndoa ya pili na Mrema, tayari ndoa yake ya kwanza ilikuwa imeshavunjika kwa mujibu wa sheria.

Mwanasiasa huyo aliyewahi kushika cheo cha Naibu Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1993 hadi 1994, pamoja na nyadhifa mbalimbali za uwaziri nchini ikiwamo Mwenyekiti wa Chama cha TLP, alifunga ndoa hiyo baada ya mke wake wa kwanza, Rose kufariki dunia tarehe 21 Septemba 2021.

KESI ya HALIMA MDEE na WENZAKE 18 KILICHOTOKEA MAHAKAMA KUU HIKI HAPA – “WAKILI AELEZA KILA KITU”..

Leave A Reply