The House of Favourite Newspapers

AWESO AWASWEKA NDANI MHANDISI, MKANDARASI, KISA HIKI HAPA! – VIDEO

Mhadisi wa Maji wa Wilaya ya Monduli, Charles Seidea, akimueleza Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kuhusu namna mradi wa maji katika kijiji cha Lendenyika wilayani Monduli.

NAIBU Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso,  ameamuru kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Monduli, Charles Saidea, na Mkandarasi kutoka kampuni ya Meru Constructions, Ayo Jeremia,  kwa tuhuma za kufanya udanganyifu katika miradi ya maji inayoendelea katika vijiji 10 vya Halmashauri ya Wilaya ya Monduli.

Aweso ametoa agizo hilo katika kijiji cha Lendenyika wakati wa ziara yake ya siku moja katika wilaya ya Monduli kukagua utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji 10 vya Halmashauri hiyo, ziara ambayo, hata hivyo, alilazimika kuikatisha baada ya kubaini kuwepo kwa taarifa zinazokinzana na taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa maji wenye thamani ya Sh Bil 1.79.

Askari akiwa amewakamata mhandisi na mkandarasi kutokana na agizo la Aweso.

Mbali na uwepo wa dosari nyingi za kiufundi, mradi huo unaotajwa kukamilika kwa asilimia 85 bado haujaanza kutoa maji huku mkandarasi akieleza kuidai serikali sehemu ya fedha za mradi huo,  jambo ambalo mhandisi alionekana kupinga uwepo wa madai hayo.

Hoja ya kuwepo kwa mabomba ya plastiki yaliyopita katika makorongo iliibuliwa na mmoja wa wakazi wa kijiji cha Lendenyika, Lemta Naisikie, baada ya kutaka kujua kama ni sahihi kwa mkandarasi kupitisha bomba hizo katika sehemu za wazi badala ya bomba za chuma.

“Swali langu ni moja; bomba zilizotandazwa kuleta maji katika kisima kuna sehem za makorongo, zote zimewekwa  bomba la mpira, hii naona ni changamoto kwani afadhali lingewekwa bomba la chuma.  Maeneo mengine kuna mawe,  tungeomba mkandarasi atandaze bomba la chuma ili zisilete athari baadaye, ”alisema Naisikie.

Baada ya kutolewa kwa hoja hiyo, Aweso aliamua kutembelea baadhi ya makorongo na kujionea bomba la plastiki likiwa limepita juu badala ya bomba la chuma,  ndipo akaamua kutoa maelekezo.

Watuhumiwa hao wakiwa kwenye karandinga tayari kuelekea kituo cha polisi.

“Viongozi wenu wote wanazungumzia suala la maji, Lendenyika ni moja ya vijiji vyenye changamoto kubwa sana ya maji. Mbunge wenu amepiga sana kelele kuhusu maji kwa wananchi wa Monduli, sasa sisi leo tumekuja hapa tumeona kuna mradi wa zaidi ya sh Bil 1.79 lakini mradi umefanyika kwa zaidi ya asilimia 80 lakini maji kwa wananchi hakuna,”  Aweso alisema na kuongeza:

Mafundi wakiendelea na uunganishaji wa Bomba za kupeleka Maji katika kijiji cha Lendenyika wilayani Monduli mkoa wa Arusha.

“Unawauliza wataalamu wetu wakupe taarifa zile sahihi hawakupi, leo mwananchi huyu wa kawaida kabisa anakupa taarifa sahihi mahala ambapo yalitakiwa kuwekwa mabomba ya chuma yameweka mabomba ya plastiki na hakuna usimamizi wa aina yoyote.”

 

Aweso akitazama namna mafundi wakiunganisha mabomba ya maji katika mradi unaopeleka maji  Kata ya Sopeko na Lendenyika wilayani Monduli, Arusha.

 

Baadhi ya wananchi wa Lendenyika wakimsikiliza Aweso (hayupo pichani) alipotembelea mradi huo.

 

Aweso akiendelea kukagua mradi huo.

 

Na Mwandishi wetu, Monduli.

Comments are closed.