The House of Favourite Newspapers

Azam Wamwekea Cioaba Mkataba Mezani

0

LICHA ya kuwepo kwa taarifa za chinichini zikimuhusisha kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba kutaka kuachana na timu hiyo uongozi wa klabu hiyo kupitia kwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Zakaria Thabith ‘Zaka za Kazi’ umeweka wazi kuwa kocha huyo ataendelea kusalia klabuni hapo kwani tayari washaanza taratibu za kumwongezea mkataba.

 

Mkataba wa Cioaba na Azam FC unatarajiwa kufikia tamati mwishoni mwa msimu huu huku ishu ya Corona ikionekana kuwa kikwazo katika dili hilo.Akizungumza na Championi Jumamosi, Zakaria alisema tayari wapo kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba na kocha Cioaba ili kumwezesha kusalia katika viunga vya Chamazi kwa kipindi kirefu zaidi.

 

“Kwa kipindi kirefu sasa klabu yetu imekuwa na utaratibu wa kubadilisha makocha mara kwa mara kabla hata hawajamaliza msimu na kama unakumbuka vizuri kocha pekee wa Azam aliyewahi kumaliza msimu ni Stewart Hall, sasa tumefanya tathimini na kuona huo siyo utaratibu mzuri kwani unakuwa ni utaratibu unaolenga malengo ya muda mfupi.

 

“Sasa hivi tumeamua kubadilisha utaratibu na tunatamani kuona tunakuwa na mwalimu mmoja kwa kipindi kirefu, hivyo tumeanza kufanya utaratibu wa kumwongezea mkataba kocha Cioaba,” alisema Zakaria.Cioaba ameiongoza Azam FC katika mechi 24 msimu huu na kukusanya pointi 45 baada ya kushinda mechi 13, amefungwa mechi tano na kutoa sare sita.

Leave A Reply