BAADA YA KUKAA MPWEKE…BABU ALILIA MKE MKUTANONI

ARUSHA: Katika hali isiyokuwa ya kawaida, babu mwenye umri wa miaka 70, mkazi wa Mtaa wa Kilimaji, Kata ya Moshono jijini Arusha, Loshiye Kivuyo, amewaduwaza wananchi waliokuwa wamefurika katika mkutano wa hadhara, pale aliposimama na kuwataka viongozi wa mtaa huo kumpatia mke kwa kuwa amechoka kuishi bila mke na ana kiu ya tendo la ndoa.  

 

Kikongwe huyo (pichani) alipata fursa ya kutoa ya moyoni mara baada ya kunyoosha kidole na kuruhusiwa kusimama katika mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita uliokuwa ukijadili masula mbalimbali ya maendeleo ya mtaa huo katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

 

Babu huyo alisema amechoka kuishi bila mke kwani hata yeye ana kiu ya tendo la ndoa na anataka kupikiwa na mke hivyo anawaomba viongozi wa mtaa huo kumtafutia mke katika mkutano huo. “Mwenyekiti mimi hapa ni mzee, nahitaji niwe na mke, nina kiu ya muda mrefu sijapata tendo la ndoa, nataka katika mkutano huu unipatie mke, nataka kulala na mke wangu leo,” alisema babu huyo.

 

Alilalama kuwa amechoka kupikiwa chakula na dada yake ila kwa sasa anataka kuwa na mke aweze kumbembeleza kwa kuwa anaamini wapo wanawake wanaompenda kwani bado yeye ni ‘handsome’ na hajachoka kama wanavyomdhania.

 

Baada ya kulalamika katika mkutano huo kwa muda usiozidi dakika tatu, gazeti hili lilimfuata babu huyo ili kujiridhisha na madai yake. Alipoulizwa iwapo alishawahi kuishi na mke na kama ana watoto, alikiri kuishi na wanawake mbalimbali, lakini walikuwa wakimwacha kwa sababu ambazo hakuziweka bayana.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Wilbert Jonas alimwelezea mzee huyo kuwa amekuwa na tabia ya kudai kupatiwa mke kila mara hapo ofisini na katika mkutano huo aliutumia kama sehemu ya kufikisha ujumbe wake.

 

Alisema wao kama viongozi hawajaanza leo kusikia kilio cha mzee Kivuyo ila alidai ni jambo geni kwa utamaduni wa nchini kwa viongozi kutafutia wananchi wao wake wa kuoa, ndiyo maana wanashindwa wafanyeje.

 

“Huyu babu Kivuyo ni mkazi wa hapa mtaani kwangu na kila mara analalamika anataka mke na sisi kama viongozi si jukumu letu kuwatafutia wananchi wake wa kuoa na mila na desturi zetu hapa nchini haziruhusu, sijawahi kusikia jambo kama hilo,” alisema mwenyekiti huyo

Loading...

Toa comment