The House of Favourite Newspapers

Baada ya Kupigwa Stop Sauzi, Wema Zari Hapatoshi

DAR ES SALAAM: Hapatoshi! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia zilipendwa wa mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Zarina Hassan na Wema Sepetu kuonesha kwamba upepo utakuwa mbaya siku watakayokutana baada ya Wema kusisitiza kwamba lazima aende Sauz katika bethidei ya mtoto wa Zari, Tiffah.

 

Kauli hiyo ilikuja mara baada ya Diamond kuwapa ofa ya tiketi za ndege kwenda Sauz kwenye bethidei ya mwanaye, wanakamati walioandaa sherehe ya arobaini ya mtoto wa mtangazaji Zamaradi Mketema, Salah.

 

NI JUMATANO ILIYOPITA

Mara baada ya Diamond kutangaza ofa hiyo katika sherehe iliyofanyika Jumatano iliyopita nyumbani kwa Zamaradi, Mabwepande jijini Dar na Wema akiwa miongoni mwa wanakamati, gumzo liliibuka kwenye mitandao ya kijamii kwamba itakuwaje zilipendwa hao wawili wakikutana?

“Kama nawaona vile watakavyopandishana na kushushana, si unajua Zari atakuwa na kigezo kwamba yeye ndiyo mwenye nyumba lakini Wema naye hawezi kuwa mnyonge maana yeye atakuwa ametoka Bongo na Diamond,” alichangia mdau mmoja mtandaoni.

 

WENGINE WAFUKUA MAKABURI

Mjadala wa Wema na Zari ulizidi kushika kasi mtandaoni kama moto wa kifuu ambapo kuna baadhi ya wachangiaji, walienda mbali zaidi kwa kukumbushia chanzo cha Zari kuachana na Diamond kwamba ilikuwa ni Wema.

Walisema, licha ya Zari kusikia maneno kwa muda mrefu kuhusu Diamond kurudiana na Wema, alicharuka zaidi baada ya kuona video ya Wema na Diamond wakishikana kimahaba walipokuwa katika shoo ya utambulisho wa msanii wa Wasafi Classic Baby (WCB), Mbosso iliyofanyika katika Hoteli Kilimanjaro Kempiski. “We unafikiri Zari ana imani na Wema? Yaani waende wote kwenye bethidei lakini si Wema, shughuli inaweza kuharibika maana Mganda ana misimamo ya hatari,” alichangia mdau mwingine mtandaoni.

 

ZARI AWAPIGA STOP

Wakati gumzo likiwa ni Wema kwenda kwenye sherehe hiyo, kupitia mtandao wa Instagram, Zari alitupia kauli iliyoonesha kuwapiga stop Wema na wanakamati wenzake baada ya picha ya wanakamati hao kuwekwa mtandaoni na kusindikizwa na ujumbe wa kuonesha kwamba wanajiandaa kwenda Sauz. “Sitaki kunichafulia nyumba kaeni hukohuko,” alikomenti Zari kwenye picha hiyo ya wanakamati akiwemo Wema.

 

WEMA ASISITIZA ANAENDA

Akizungumza na mwanahabari wetu, Wema alisisitiza kuwa yeye atakwenda kwenye bethidei ya Tiffah kwani ameshazungumza mara kwa mara kuwa hana tatizo na Zari isipokuwa watu wanakuza mambo.

Alisema, mara nyingi amekuwa akisema uhusiano wake na Diamond ulishaisha, wamebaki kuwa kama marafiki hivyo kamwe hawezi kuwa na kinyongo na Zari hata siku moja. “Mimi nitaenda Sauz kama nilivyoalikwa kwa baby Tiffah, hayo mengine mimi siyajui. Sina kinyongo na Zari nimeshasema jamani mara kwa mara na ninarudia tena leo, sina kinyongo,” alisisitiza Wema.

 

KITENDAWILI KUTEGUKA LINI?

Kitendawili cha itakuwaje kama Wema ataendelea kushikilia msimamo wake wa kwenda kitateguliwa Agosti 17, mwaka huu siku ambayo imepangwa kufanyika bonge la pati la Tiffah Sauz, nyumbani kwa Zari hivyo mashabiki watajua mbivu na mbichi endapo Wema ataenda.

Siku hiyo pia imetajwa kuwa moja ya siku ambayo huenda Diamond akaitumia kumaliza tofauti na mwandani wake Zari waliyemwagana Februari 14, mwaka huu kwa kile alichoeleza Zari kuwa ni Diamond kutawaliwa na skendo za wanawake tofauti.

 

TUJIKUMBUSHE

Awali, Diamond aliahidi kuwalipia tiketi watu 30 kwa ajili ya kuhudhuria sherehe hizo lakini baadaye aliongeza kuwa atawalipia watoto 10 pamoja na wazazi wao ili nao wahudhurie sherehe hizo.

Katika kunogesha sherehe hizo, juzi Jumatano wakati wa sherehe ya kufikisha siku 40 ya mtoto wa mtangazaji Zamaradi Mketema, mwanamuziki huyo alialika wanakamati zaidi ya 10 kuhudhuria sherehe hiyo.

Tiffah ambaye jina lake halisi ni Latiffah alizaliwa Agosti 6, 2015. Hata hivyo, sherehe za kuzaliwa binti huyo zimesogezwa mbele kutokana na ratiba ya shoo za Diamond nje ya nchi ambapo sasa itafanyika siku tatu mfululizo kuanzia Agosti 17-19 mwaka huu.

STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Jumamosi

Comments are closed.