The House of Favourite Newspapers

Baada ya Kutiwa Mbaroni… Utajiri Nabii Bilionea Waibuliwa

0

SI habari tena kwamba, mchungaji maarufu wa Kanisa la Enlightened Christian Gathering (ECG), Nabii Shepherd Bushiri, ametiwa mbaroni kwa tuhuma za ukatatishaji wa fedha haramu, lakini habari kubwa ni juu ya utajiri wake wa kutisha ambao umeibuliwa.

 

Kwa mujibu wa Jarida la Forbes Africa, Nabii Bushiri wa kanisa hilo lililopo maeneo ya Makongo-Juu jijini Dar na makao yake makuu yakiwa Lilongwe nchini Malawi, anatajwa kwenye orodha ya wachungaji mabilionea zaidi barani Afrika.

 

MSALA WA KUTIWA MBARONI

Kwa mujibu wa vyombo vikubwa vya habari vya kimataifa, Nabii Bushiri na mkewe, Marry Zgambo walitiwa mbaroni mapema Jumanne wiki hii, nyumbani kwake, Pretoria nchini Afrika Kusini.

 

Imeelezwa kuwa, Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai, Uchumi na Rushwa (Hawks) cha nchini Afrika Kusini, ndicho kiliwatia korokoroni kwa tuhuma hizo za kutakatisha Rand (Fedha za Afrika Kusini) milioni 102 sawa na takriban shilingi bilioni 14 za Kitanzania.

 

Bushiri na mkewe ambao wamejaaliwa watoto wawili, walikamatwa baada ya kudaiwa kujaribu kuikwepa timu hiyo ya Hawks iliyokuwa ikiwasaka, hivyo baada ya kukamatwa waliongozana na timu hiyo kuelekea Kituo cha Polisi cha Silverton jijini Pretoria na kikundi cha mawakili wao.

 

Taarifa ya kanisa hilo ambayo ilitolewa kabla ya kukamatwa, ilisema kwamba, waliarifiwa na mawakili wa Bushiri siku ya Jumatatu kuwa, Hawks waliomba kiongozi wao afike katika ofisi zao kuhusiana na uwekezaji wake unaohusiana na kampuni yake inayoitwa Rising Estate.

 

Imeelezwa kwamba, hii ni mara ya pili kwa mchungaji huyo na mkewe kutiwa mbaroni kwa makosa kama hayohayo.

Mara ya kwanza walikamatwa Februari, 2019 kwa tuhuma za kutakatisha Randi milioni 15 sawa na takriban shilingi bilioni 2.12 za Kitanzania.

 

Wakati huo inaelezwa kwamba, Bushiri alijisalimisha mwenyewe Polisi nchini Afrika Kusini baada ya mkewe kukamatwa. Walishafikishwa mahakamani, lakini kabla ya kesi hiyo kufika tamati, wamekamatwa tena kwa msala kama huohuo.

 

Katika kesi mpya, wawili hao walifikishwa mahakamani juzi Jumatano ambapo kesi yao iliahirishwa hadi Oktoba 30, mwaka huu huku wenyewe wakiendelea kusota mahabusu bila dhamana.

 

UKWASI WA KUTISHA

Nabii Bushiri anatajwa kuwa mmoja wa viongozi wa dini wenye ukwasi wa kutisha, lakini wenye viulizo vya namna alivyoupata. Jamaa huyo amekuwa akitiliwa shaka kutokana na utajiri wake huo ambao chanzo chake hakieleweki.

 

Yeye binafsi amekuwa akieleza kuwa anamiliki biashara nyingi zinazomuingizia kipato kikubwa, ikiwemo kuuza mafuta ya upako na uwekezaji katika mahoteli na makampuni ya kifedha.

 

Nabii Bushiri amekuwa akiishi maisha ya kifahari mno (lavish life) pamoja na familia yake huku akimiliki mali nyingi kama majumba ya kifahari, mahoteli, magari ya bei mbaya, ndege binafsi na mambo mengine yaliyojaa kufuru ya fedha kama anavyojionesha kwenye mitandao ya kijamii.

 

Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko ya watu kadhaa wakidai kudhulumiwa fedha, madini na mali nyingine za thamani na mtu wanayemtaja kwa jina la Nabii Bushiri.

 

Inaelezwa kwamba, malalamiko hayo ndiyo yaliyosababisha Polisi wa upelelezi nchini Afrika Kusini kuanza kumfuatilia yeye na mkewe na kugundua kuwa, kwa pamoja wamekuwa wakijihusisha na utakatishaji wa fedha haramu zitokanazo na sadaka za kanisa.

 

Nabii Bushiri ambaye pia ni maarufu kwa jina la Major 1, kwa mujibu wa Mtandao wa Indapaper. com, hadi mwaka jana, utajiri wake ulikadiriwa kufikia Dola za Kimarekani milioni 170 (zaidi ya shilingi bilioni 389 za Kitanzania).

 

Vyanzo vya mapato vinavyoonekana katika historia yake ni umiliki wa Chuo Kikuu cha Kilimo, uwekezaji katika nyanja ya mawasiliano, umiliki wa migodi ya dhahabu na makanisa ambayo yana matawi katika nchi za Tanzania, Afrika Kusini, Botswana na Namibia.

 

Mbali na Nabii Bushiri, wachungaji wengine maarufu barani Afrika wanaotajwa kuwa na utajiri usiokuwa wa kawaida ni pamoja na Chris Okotie, Matthew Ashimolowo, Temitope Joshua ‘TB Joshua’, wote hawa kutoka Nigeria na wengine wengi.

 

STORI: SIFAEL PAUL

Leave A Reply