The House of Favourite Newspapers

Baada ya Manenomaneno… Meneja wa Kiba Apasua Jipu!

0

KUMEKUWA na minong’ono mingi kwenye mitandao ya kijamii kufuatia staa wa Bongo Fleva, Ali Saleh KibaKing Kiba’ kuonekana karibu na mrembo, Esi Mgimba, kiasi cha wengine kudai wana uhusiano wa kimapenzi, lakini mrembo huyo amepasua jipu pwaa, IJUMAA linakupa zaidi.

 

AMEMPINDUA SEVEN?

Katika maneno hayo ya mitandaoni, kuna baadhi ya watu walikwenda mbele zaidi na kudai kuwa, Esi ndiye meneja mpya wa Kiba ambaye amempindua aliyekuwa meneja wake, Christine Mosha ‘Seven’ waliyedaiwa kutengana hivi karibuni.

 

Kufuatia mkanganyiko huo mitandaoni, Gazeti la IJUMAA lilijipa jukumu la kumtafuta mrembo huyo ambaye awali alikuwa akifanya kazi za ofisa mawasiliano na uhusiano wa kijamii (Communication and Public Relation Officer) na Ushauri wa Kibiashara (Business Consultant).

 

ESI AFUNGUKA

Esi ambaye ni maarufu kwenye mitandao ya kijamii kwa jina la Esilovey alianza kwa kufungukia cheo chake kwa Kiba huku akikanusha kuchukua nafasi ya Seven.

 

“Mimi cheo changu ni Music Talent Manager and Business Consultant wa Kiba. Sifanyi hivyo kwa Kiba tu, bali hata Kings Music Records (lebo ya muziki inayomilikiwa na Kiba).”

 

NI MARAFIKI WA MUDA MREFU

Esi alisema kuwa, yeye na Kiba ni marafiki wa muda mrefu na walikuwa na maelewano mazuri tangu zamani.

 

“Tunaendana, sisi ni marafiki wa muda mrefu, hatujajuana leo. Mimi nilikuwa ninafanya kazi nyingine kabisa, lakini Kiba alikuja, akaniambia tufanye kazi pamoja.

“Kwa kuwa ninamjua Kiba kwa muda mrefu, najua ni mtu mzuri ambaye kusema kweli ana moyo safi sana, nikaona amenipa heshima kubwa.”

 

KUHUSU MADAI YA MITANDAO

Mrembo huyo mwenye umbo kubwa na la kuvutia alisema watu wamekuwa wakiongea mengi kumhusu yeye na Kiba jambo ambalo halina ukweli wowote, kinachowaunganisha wao ni kazi na urafiki wa kawaida.

 

“Mitandaoni wanaongea mengi huwezi watu kuwazuia lakini ukweli mimi ni meneja na rafiki wa kawaida, hakuna zaidi ya hilo,” alisema.

 

FURAHA KAMA YOTE

Esi hakusita kueleza ni kwa jinsi gani alivyo na furaha kama yote kufanya kazi na staa mkubwa kama Kiba. “Nina furaha sana kufanya kazi na Kiba,” alisema Esi.

 

ATANGAZA MATARAJIO KWA MASHABIKI

Meneja huyo mpya wa Kiba hakusita kueleza mategemeo na matarajio yake kwa mashabiki wa Kiba.

“Mashabiki wa Kiba wajue, huu ni wakati wa watu ku-enjoy (kufurahia) muziki mzuri kutoka kwa King Kiba,” alisema.

 

Esi ameahidi kufanya makubwa na Kiba ambayo kimsingi yatakwenda kuleta mapinduzi katika Bongo Fleva na Kiba atakuwa anaachia ngoma baada ya ngoma.

 

KUHUSU FAMILIA YA KIBA?

Akizungumzia mambo ya mitandao juu ya masuala binafsi ya Kiba na yeye, Esi alisema kuwa, watu wanapaswa kutofautisha kazi na mambo ya kifamilia.

 

“Mimi ningeomba tujitahidi sana kutofautisha kazi na familia. Ningeomba tuzungumze kazi, masuala ya Kiba na familia yake tumwachie yeye mwenyewe kwani hayahusiani na kazi,” alisema Esi.

 

SHOO YA MWANZA

Kuhusu kusitishwa kwa shoo ya Kiba jijini Mwanza iliyotarajiwa kufanyika hivi karibuni, Esi alisema suala hilo lilitokana na kuwepo kwa maandalizi ya Sherehe za Uhuru (keshokutwa, Desemba 9) zitakazofanyika kitaifa jijini humo.

 

“Nadhani kuna zoezi la kitaifa ndiyo maana iliahirishwa, lakini tutaitangaza hivi karibuni baada ya mambo kukaa sawa,” alisema Esi.

 

ESI ANAJUA KUAMSHAAMSHA

Kwa mujibu wa watu waliozungumza na IJUMAA, Esi anajua mno kuamshaamsha hasa kwenye mitandao ya kijamii hivyo ni chaguo sahihi kwenye menejimenti ya Kiba.

 

“Esi ni mchangamfu sana, anajua kuamshaamsha na hivyo ndivyo muziki wa Bongo Fleva unavyotaka, tofauti na Seven ambaye ni mpole na ni mtu wa mikakati zaidi kuliko harakati. Lakini Esi anapiga kotekote, kwenye mikakati na harakati. Hope (natumaini) atamfikisha Kiba mbali,” alisema Eva, mkazi wa Mwananyamala-Komakoma anayemfahamu fika Esi.

 

Esi anatarajia kumuongoza Kiba katika shoo ya kihistoria ya Fiesta inayotarajia kufanyika kesho kutwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar ambapo mkali huyo anatarajiwa kufanya shoo ya kipekee itakayoacha historia ya kuvungia mwaka 2019.

Stori: Imelda Mtema, Dar

 

Rais Magufuli Akiweka Jiwe La Msingi Ujenzi Wa Daraja La Kigongo Busisi

Leave A Reply