The House of Favourite Newspapers

Baada ya Mkataba Kuisha, Pogba Aondoka na Sh bilioni 11 Man United

0
Pogba ameondoka na donge nono la bilioni 11 Manchester United

IMEFICHUKA kuwa Paul Pogba ataondoka na bonasi ya pauni milioni 3.78 (Sh bilioni 11) atakapoachana na Manchester United mara baada ya mkataba wake kufikia tamati mwishoni mwa mwezi huu.

 

United ilithibitisha juzi Jumatano kuwa kiungo huyo Mfaransa ataondoka Old Trafford mkataba wake utakapomalizika Juni 30, huku pia ikithibitishwa kuwa Jese Lingard naye anasepa.

 

Licha ya kuwa na kiwango duni na majeraha ya mara kwa mara katika misimu yake miwili ya mwisho, Pogba atapewa posho ya utumishi, pauni milioni 3.78, kama walivyokubaliana kwenye mkataba.

Pogba anawindwa na waajiri wake wa zamani klabu ya Juventus

Hiyo siyo habari itakayopokelewa vizuri na mashabiki wa Man United ambao hawajaona ubora wa mshindi huyo wa Kombe la Dunia tangu arejee kwa mara ya pili Old Trafford akiwa amecheza kwa miaka sita hadi sasa.

 

Nyota huyu rasmi amekuwa hasara kwa United ambayo ilimlipa dau la usajili wa rekodi ya dunia, pauni 89m, alipokuwa akirejea kutokea Juventus mwaka 2016, baada ya kumpoteza kwa Waitaliano hao kwa kulipwa fidia ya pauni 1.5m tu mwaka 2012.

 

Kwa sasa Paul Pogba ni mchezaji huru anayeweza kusaini na timu yoyote ile ingawa waajiri wake wa zamani klabu ya Juventus inawinda saini yake

Licha ya kulipa kitita hicho kikubwa, United pia ilimlipa wakala wa mchezaji huyo, marehemu Mino Raiola pauni 39.27m (Sh bilioni 114).

 

Pogba pia alikuwa akilipwa kwa mwaka mshahara wa pauni 7.75m (Sh bilioni 22.5), malipo ya haki za matangazo pauni 2.87m (Sh bilioni 8.4) na posho ya pauni 1.875m (Sh bilioni 5.4) katika kila msimu, kwa misimu minne ambayo United ilifuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.

 

Licha ya kuwekeza fedha zote hizo, United haitaambulia chochote kwa Pogba, kwa kuwa anaondoka bure.

Leave A Reply