The House of Favourite Newspapers

Baba Amuua Mpenzi wa Binti Yake kwa Kipigo

0

 

MAKACHERO kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) nchini Kenya wamemkamata mwanamme aitwaye John Christon Shipiti (52) kwa madai ya kumuua mwanafunzi wa darasa la nane aliyedai alikuwa anamnyemelea bintiye.

 

 

Ripoti zilionyesha kwamba Shipiti alimshambulia mwanafunzi huyo wa miaka 17 kutoka shule ya msingi ya Chemego kwa tuhuma za kumnyemelea bintiye mwenye umri wa miaka 13.

 

 

Kulingana na ripoti ya DCI, marehemu alipata majeraha makubwa na aliripotiwa kufariki dunia wakati alipofikishwa katika hospitali ya Vihiga kutibiwa.

 

 

“Mwathiriwa aliachwa na majeraha makubwa miguuni, katika paji la uso, mashavuni na mdomoni baada ya kupata kichapo. Kisa hicho, hata hivyo, kilifichwa hadi jana,” ripoti ya DCI ilisema.

 

 

Polisi walisema mshukiwa atasalia korokoroni akisubiri kufikishwa mahakamani.

 

 

Na katika kisa kingine cha kutisha, baba wa binti wa umri wa miaka 18 alikamatwa  kwa madai ya kumdunga kisu mpenzi wa msichana wake.

 

 

Ripoti ilisema kwamba mzee huyo mwenye umri wa miaka 61 alimdunga kisu mvulana huyo baada ya kumfumania bomani mwake akiwa na bintiye. Mshukiwa yuko kituo cha polisi wakiendelea na uchunguzi.

 

 

Visa hivyo vinajiri wakati idara ya DCI imetangaza kukaza kamba katika kukabili visa vya uhalifu nchini. DCI ilizindua nambari ya simu bila malipo ya 0800722203, ambayo umma unaweza kuitumia kuripoti uhalifu kwa idara hiyo bila kutambulika. Hatua hiyo inakusudiwa kuhakikisha kuwa visa vya uhalifu vinawafikia polisi haraka iwezekanavyo.

Chanzo -Tuko News.

 

Leave A Reply