The House of Favourite Newspapers

BABA DIMPOZ: MWANANGU KALOGWA…

Faraji Nyembo

BAADA ya madai kuzagaa kwamba staa wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ amelogwa na siyo suala la kulishwa sumu kama yeye anavyoamini, baba yake mzazi wa mwanamuziki huyo, Faraji Nyembo amefunguka kuwa kama ni kulogwa basi mwanaye huyo kalogwa Kizungu.  Akizungumza na Ijumaa kwa njia ya simu akiwa Tabora, baba Dimpoz alisema yeye haamini kama kuna uchawi wa tunguli kwani ni mambo ya kizamani bali kwa sasa kuna kulogwa zaidi Kizungu ambapo mtu anaweza kukushika tu mkono kumbe ameshakuwekea sumu tayari.

“Naamini Dimpoz hajalogwa kwa njia ile inayofahamika kama watu wanavyosema, siku hizi kuna uchawi wa Kizungu ambapo mtu anakupa mkono au kipaza sauti kumbe kina sumu.

“Nawasihi watu wasiamini sana katika uchawi maana kama Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe wakati alipopata matatizo ya kuugua ingeaminika ni uchawi tungempoteza, lakini alienda kwa madaktari na alipona,” alisema baba Dimpoz.

Aliendelea kusema kuwa, mastaa kama Dimpoz, Diamond, Ali Kiba na Nay wa Mitego wanatakiwa kuwa makini sana kila wanapokuwa, tena ikiwezekana wawe na walinzi maalum wa kutembea nao kila kona kwa ajili ya usalama wao. “Hawa mastaa wanatakiwa kuwa makini kwa kila kitu, wasiwe wanakula au kunywa sehemu bila kuwa na tahadhari maana wao ni watu maarufu, lazima wanakuwa na marafiki pia maadui wengi.

“Najua mwanangu Dimpoz atakuwa amejifunza na naamini atapona kwa uwezo wa Mungu, hii ni vita tu ya kidunia itapita na akishapona atakuwa mwangalifu zaidi maana mtu hujifunza kutokana na makosa,” alisema baba Dimpoz.Kwa upande mwingine baba Dimpoz alisema anatamani sana kwenda kumuona mwanaye Afrika Kusini alipo kwa matibabu lakini anashindwa kutokana na kwamba hana nauli ya kufika huko.

“Namuombea mwanangu usiku na mchana ili Mungu amponye arudi kwenye muziki kama kawaida na kwa uwezo wake atapona, pia natamani sana kwenda kumuona lakini sina uwezo na naamini angeshangaa na angefurahi sana kuniona,” alisema.

Hivi karibuni Dimpoz alieleza kuwa chanzo cha ugonjwa unaomsumbua kwa mujibu wa madaktari ni kunywa kimiminika chenye sumu ambayo imeharibu mfumo wake wa chakula hivyo kufanyiwa upasuaji wa njia nyingine ambapo mpaka sasa hali yake haijatengemaa.

STORI: Gladness Mallya, Ijumaa

Comments are closed.