The House of Favourite Newspapers

Baba Mzazi Adaiwa Kumfanyia Unyama wa Kutisha Mwanaye!

0
Mtoto mwenye umri wa miaka 6, anayedaiwa kumfungwa kamba mikononi na miguuni kisha kumfungia ndani na baba yake aliyejulikana kwa jina moja la Mushi.

INAUMA SANA! Baba aliyejulikana kwa jina moja la Mushi, mkazi wa Namanga- Msasani jijini Dar, amemfanyia unyama wa kutisha mtoto wake wa kumzaa, (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 6, kwa kudaiwa kumfunga kamba mikononi na miguuni kisha kumfungia ndani.

Habari za kusikitisha zilizofika kwenye meza ya gazeti hili zilidai kuwa, baba huyo amekuwa na tabia ya kumfungia ndani mtoto huyo kuanzia asubuhi mpaka jioni anaporudi kwenye kazi zake, jambo ambalo limekuwa likiwaumiza majirani zake.

Akifunguliwa kamba mikononi na miguuni.

SHUHUDA AZUNGUMZA

Akizungumza na Uwazi, shuhuda wa tukio hilo ambaye ni mmoja wa majirani wa baba huyo (jina linahifadhiwa) aliliambia gazeti hili kuwa, mara nyingi walikuwa wakisikia sauti ya mtoto akilia kwa muda mrefu kutoka ndani ya chumba cha baba huyo wakati huohuo hawakuwa wanamuona mtoto Brian akicheza nje na wenzake kama zamani.

Aliendelea kudai kuwa, kipindi cha nyuma baba huyo ambaye ametengana na mama wa mtoto huyo, alikuwa akimfungia mwanaye ndani lakini akiondoka mtoto huyo anafungua mlango na kujumuika na wenzake.

“Mara nyingi tunakuwa tunasikia mtoto analia ndani kwa muda mrefu sana akisema ‘nakufaa… nisaidieni…’ na pia hatukuwa tunamuona akitoka nje kucheza na wenzake kama zamani,” alidai jirani huyo na kuongeza:

“Unajua huyu baba anaishi na mtoto wake bila mama, sasa kila mara anamfungia na kudai eti ni mtundu sana, anamshindisha njaa siku nzima, sisi kama wazazi tulishangazwa sana na tabia hiyo.”

WATOTO WENZAKE NAO WANENA

Jirani huyo alisema watoto wao ndiyo walikuwa wakiwaambia mara kwa mara kuwa mwenzao huyo anakatazwa na baba yake kucheza nao, hivyo amekuwa akifungiwa ndani mchana kutwa.

WAZO LA KWENDA POLISI

Alisema siku ya tukio waligundua mtoto huyo kafungiwa ndani kama kawaida baada ya kusikia akilia kwa muda mrefu akiomba msaada, ndipo walipojikusanya na kuwa na wazo la kufikisha ishu hiyo polisi.

“Kwa kweli uvumilivu ulitushinda, tulimsikitikia sana yule mtoto, tuliona anachofanyiwa tena na baba yake mzazi siyo sawa, hata kama ni mtundu lakini hakustahili kufanyiwa ukatili huo, tulichoamua ikawa ni kwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Oysterbay, nao bila hiyana walifika eneo la tukio na kuona hali halisi.”

Mtoto huyo baada ya kuokolewa.

POLISI WAVUNJA MLANGO

“Kwa kufuata taratibu, polisi walivunja mlango na kumkuta mtoto huyo akiwa uchi wa mnyama huku akiwa amefungwa kamba miguuni na mikononi kwa nyuma na puani katapakaa kamasi na alionekana kutokwa na jasho jingi. Inauma sana,” alisema jirani huyo.

Aliongeza kuwa, baada ya kuona hivyo kama wazazi waliumia sana na kuamua kumsindikiza mtoto huyo katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar wakiwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.

BABA ATOWEKA

Shuhuda huyo aliongeza kuwa walipofika polisi waliambiwa jeshi hilo litamsaka baba wa mtoto huyo, hata hivyo taarifa zinasema Mushi aliposikia kwamba mwanaye amechukuliwa na polisi alitoweka mpaka leo hajulikani alipo.

MAMA WA MTOTO AFUNGUKA

Gazeti hili lilipata fursa ya kuzungumza na mama wa mtoto huyo ambapo alisema amewasili jijini Dar akitokea Moshi kuja kumchukua mwanaye baada ya kusikia yanayompata kutoka kwa baba yake.

“Unajua mimi nilitengana na huyo baba yake muda mrefu, lakini cha ajabu alimtuma mdogo wake kuja kumuiba huyu mtoto nyumbani kwetu.

“Baada ya mtoto huyo kuletwa Dar kwa baba yake nikawa napigiwa simu na majirani zangu mara kwa mara na kuambiwa kuwa mwanangu anateseka sana.

“Kama mama niliumia sana, nikaona nina kila sababu ya kuja kumfuata ndipo nikamkuta polisi na kukabidhiwa huku baba yake akiendelea kusakwa.

“Inasikitisha, kwa nini alikuwa anamfunga kamba na kumfungia ndani? Imeniuma sana. Nimekuja Dar kuja kumchukua mwanangu, hakika nimeumia mno moyoni,” alisema mama huyo.

POLISI NAO WANENA

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, SACP Suzana Kaganda hakuweza kupatikana jana lakini ofisa mmoja wa polisi wa Oysterbay aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini kwa kuwa siyo msemaji, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, akasema baba wa mtoto huyo anatafutwa ili ajibu tuhuma hizo na upelelezi ukikamilika aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Ni unyama wa kutisha aliokuwa akifanyiwa huyu mtoto lakini polisi tutahakikisha baba yake anakamatwa na sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine wanaowatesa watoto wao,” alisema ofisa huyo.

STORI: IMELDA MTEMA, DAR

Leave A Reply