The House of Favourite Newspapers

Babu Pluijm atimuliwa Yanga

Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge | CHAMPIONI | DAR ES SALAAM

RASMI Yanga imemtimua mkurugenzi wake wa ufundi, Hans van Der Pluijm kwa kile kilichoelezwa kuwa kubana matumizi na kuendana hali halisi ya kiuchumi nchini kwa sasa. Pluijm aliyekuwa kocha wa Yanga kabla ya kupanda cheo na kuwa mkurugenzi wa ufundi, hadi anaachishwa kazi alikuwa na mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo.

Bosi mmoja mkubwa na mwenye ushawishi ndani ya Yanga, alilithibitishia Championi Jumamosi kwa kusema; “Ni kweli tumeamua kuachana na Pluijm kwa mambo mawili, kwanza hali ya kiuchumi. “Pili ni kuweka amani ndani ya timu maana mambo yalikuwa mengi, hivyo tumeona bora tuachane naye na katibu mkuu (Charles Mkwasa) ndiye tuliyempa jukumu la kumtaarifu Pluijm kuhusu hali hii.

“Kubaki na Pluijm ni gharama kubwa na kama unavyoona hali ya uchumi sasa si nzuri sana na tumeona busara kuachana naye ili mambo mengine yaende.” Miongoni mwa gharama ambazo Yanga imekuwa ikiingia kwa kuwa na Pluijm ni kumlipa mshahara wa dola 10,000 zaidi ya Sh milioni 22 kwa mwezi, pia gharama nyingine za nyumba na usafiri.

Alipotafutwa na gazeti hili, Pluijm ambaye ni kipa wa zamani wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 68, alisema: “Naomba jambo hilo aulizwe katibu mkuu wa timu, mimi sina la kusema.”
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Mkwasa, simu yake iliita mara tatu bila ya kupokelewa hadi jana jioni tulipoenda mitamboni.

Pluijm mwenye watoto wawili Jurgen Francois van der Pluijm na Andrea-Marie van der Pluijm, ambaye amemuoa Josephine Delali raia wa Ghana ameipa Yanga mataji mawili mfululizo ya Ligi Kuu Bara katika misimu miwili iliyopita ya ligi hiyo. Msimu uliopita, Pluijm aliiwezesha Yanga kucheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Comments are closed.