The House of Favourite Newspapers

Jitihada za RC Makonda Zimeuleta Uwanja Huu wa Soka wa Bandari, Dar

 

RC Makondana Balozi wa China nchini Tanzania, Dr. Lu Youqing wakizindua mradi huo.

Bila shaka kila mmoja wetu anakumbuka ahadi ya RC Makonda aliyoitoa mwaka jana ya kujenga viwanja vitatu (3) vya mpira kwa ajili ya maendeleo ya mashindano mbalimbali ya michezo ikiwemo Ndondo Cup kwani mashindano haya kwa ujumla wake yanalenga kuboresha mazingira ya michezo na kuzalisha vipaji vingi zaidi ambavyo vinabeba ajira nyingi za vijana ndani yake.

Kimsingi RC Makonda hakuishia tu kuahidi bali alikwenda mbali zaidi na kumualika Balozi wa China nchini Tanzania, Dr. Lu Youqing kushuhudia hali halisi ya viwanja vinavyotumika kwa sasa kama sehemu ushahidi wa kile alichokuwa amemueleza wakati akimshawishi.

Ikiwa imepita miezi kadhaa tangu Balozi kukubaliana na ombi la Mkuu wa Mkoa, jana Machi 3, 2017 Balozi huyo wa China akiwa na RC Makonda wameweka historia mpya baada ya kuweka jiwe la msingi la kuanza ujenzi wa viwanja hivyo, huku wakianza na kiwanja cha Bandari ambacho kitagharimu Dola za Kimarekani 450,000, huku kikijengwa kwa viwango vya kimataifa na kampuni iliyojenga uwanja wetu wa taifa.

Kuonyesha kutambua utendaji na msukumo mkubwa wa RC Makonda katika kutimiza azma ya Rais John Pombe Magufuli ya kutatua changamoto za wanyonge, Balozi pia amemuahidi Mkuu wa Mkoa kufanya yafuatayo:

1. Kuwapatia kipaumbele cha ajira vijana wote watakaoshiriki mashindano ya Ndondo Cup kwenye kampuni mbili za nchi hiyo ambazo zinatarajia kuanza shughuli zake hivi karibuni huku wakitarajia kuajiri zaidi ya vijana 24,000

2. Kuipeleka nchini China timu itakayoshinda michuano hiyo ili ikacheze mechi za kirafiki kama sehemu ya kuwaongezea ujuzi wa soka.

3. Kama haitoshi, timu ya pili na ya tatu kwenye mashindano zitapewa mualiko rasmi kwenye ubalozi wa nchi hiyo.

Kwa namna ya kipekee RC Makonda amemshukuru Balozi huyo kwa kuwa sehemu ya watu ambao wamechangia maendeleo ya jiji la Dar es Salaam na hivyo shughuli za maendeleo ambazo hazikuwepo kwenye bajeti ya serikali kuweza kufanyika pia.

Comments are closed.