The House of Favourite Newspapers

Balozi wa Heshima wa Visiwa Vya Shelisheli Atembelea Ofisi za OSHA

0
Balozi wa Heshima wa Seychelles nchini, Bi. Maryvonne Pool (kushoto)  akiteta jambona na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda.

 

Balozi wa Heshima wa Seychelles nchini, Bi. Maryvonne Pool, ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika usimamizi wa sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi yenye lengo la kulinda nguvukazi ya Taifa.

 

Ametoa pongezi hizo leo alipotembelea ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa lengo kufanya usajili wa moja ya miradi ambayo ofisi yake ni mbia pamoja na kujifunza namna ambavyo taasisi ya OSHA inatekeleza majukumu yake.

Aidha, Balozi huyo ameahidi kushirikiana na OSHA katika kuviwezesha vikundi vya wakulima wadogo wanaofanya shughuli zao katika wilaya za pembezoni mwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani hususan kuhakikisha kwamba vikundi hivyo vinasajiliwa na OSHA kwa ajili ya kuendelea kupatiwa miongozo ya namna ya kujikinga na madhara yatokanayo na shughuli za kilimo.

 

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema Taasisi yake imefarijika kutambua kwamba juhudi za serikali za kulinda nguvukazi ya Taifa zinaonekana.

Katika ziara yake Balozi huyo alifanikiwa kusajili mradi ambao ofisi yake ni mbia na kupatiwa cheti cha usajili papo hapo. Aidha, alipata fursa ya kubadilishana uzoefu na Mtendaji Mkuu wa OSHA kuhusu mifumo ya usimamizi wa masuala ya Usalama na Afya baina ya Tanzania na Visiwa vya Seychelles ambapo alieleza kuwa nchi yake ina sheria kali zinazohusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

 

Miongoni mwa majukumu ya OSHA ni kusajili sehemu za kazi na kisha kuendelea kuzitembelea sehemu hizo kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kutoa ushauri wa viwango stahiki vya Usalama na afya vinavyopaswa kuzingatiwa.

Leave A Reply