Banka Amhofia Makame

Kiungo mkabaji wa Yanga, Issa Mohammed ‘Banka’.

KIUNGO mkabaji wa Yanga, Issa Mohammed ‘Banka’, amejiondoa kwenye vita ya namba na Abdulaziz Makame ‘Bui’ huku akisema nyota huyo ndiyo kwanza gari limeweka.

Kauli ya Banka aliitoa mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

 

Katika mchezo huo, Makame alianza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo akicheza namba sita aliyokuwa anaicheza awali Banka ambaye yeye alitupwa saba.

 

Abdulaziz Makame.

Akizungumza na Championi Jumatano, Banka alisema kuwa Makame ndiyo nafasi yake sahihi anayoicheza akiwa Mafunzo FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar, pia kwenye timu ya taifa hivyo hana shaka na uwezo wa nyota huyo.

 

Banka alisema kuwa bado kiungo huyo hajaonyesha uwezo wake ule anaoufahamu yeye kutokana na kukosa mechi fitnesi huku akimpa muda zaidi kwa ajili ya kurejesha kiwango chake anachokijua.

 

Aliongeza kuwa hahofii kuwekwa benchi na Makame, lakini anaheshimu uwezo wa kiungo huyo mwenye uwezo wa kukaba kwa kutumia nguvu, akili huku akichezesha timu ndani ya wakati mmoja.

 

“Sihofii kiwango cha Makame ambacho labda kitaniweka benchi, mimi ninaheshimu uwezo wake na hilo lipo wazi ni kati ya viungo bora kwangu hapa nchini.

 

“Kwa mimi ninayemfahamu Makame kile kiwango alichokionyesha mechi na Zesco bado, licha ya mashabiki kusifia kiwango chake, hapo ndiyo kwanza gari limeweka subiria kumuona akionyesha kiwango zaidi ya hicho ambacho amekionyesha.

 

“Namba sita ndiyo nafasi yake anayoicheza, awali alikuwa hapati nafasi ya kucheza na mimi nimeanzishwa katika kikosi cha kwanza nikicheza namba sita kutokana na yeye kukosa mechi fitnesi ambayo tayari imeanza kurudi taratibu, hivyo Wanayanga wasubirie mengi kwake,” alisema Banka.


Loading...

Toa comment