The House of Favourite Newspapers

Baraza: Yanga Vs Kagera Ni Vita Kubwa

0

KUELEKEA mchezo wa Kagera Sugar dhidi ya Yanga kwenye raundi ya 16 ya Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Kagera, Francis Baraza amesema kuwa kikosi kinaendelea na maandalizi ya vita kubwa ya kusaka pointi tatu mbele ya vinara hao wa ligi mchezo huo unatarajiwa kupigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

 

Ikumbukwe kuwa, mara ya mwisho Yanga na Kagera Sugar walikutana kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Bara ambapo Kagera Sugar ilichapwa 1-0, Uwanja wa Kaitaba kwa bao la Feisal Salum.

 

Baraza ambaye timu yake imepanda hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 20, amesema: “Maandalizi yanaendelea vizuri, vijana wana morali kubwa kuelekea mchezo huu, wanatambua ugumu na umuhimu wa mechi hii pamoja na malengo ya timu kiujumla na naamini kuwa watapambana kwenye mchezo huu na michezo mingine ijayo kuhakikisha wanaipatia timu ushindi wa pointi tatu.

 

“Yanga ni timu nzuri, kwa hivyo itakuwa ni mechi ngumu sana na nitahitaji kupanga kikosi cha wachezaji wakomavu kimpira ambao najua watafuata maelekezo yangu kwa urahisi na kuendana na kile ambacho nitakihitaji kwenye mchezo huo.

 

“Sisi ni wawindaji kwenye mchezo huu ambapo tunatakiwa tumuwinde mnyama porini na kufanikiwa kumshinda, hivyo mimi kama Kocha Mkuu natambua kuwa mchezo utakuwa mgumu sana lakini nitahakikisha nafanya kila ninaloweza kupata matokeo ya ushindi.”

 

Katika mchezo huo, fowadi Hamis Kiiza anatarajiwa kuikabili timu yake ya zamani ya Yanga, baada ya kuifunga Simba kwenye Uwanja wa Kaitaba, hivi karibuni.

Stori: Naila Shomari

Leave A Reply