The House of Favourite Newspapers

Barrick: Kampuni ya Twiga ni ‘Ushirikiano wa Ushindi

0
Mtendaji  Mkuu wa kampuni ya Barrick Gold, Mark Bristow.

 

MTENDAJI Mkuu wa kampuni ya Barrick Gold, Mark Bristow, ushirikiano uliopo katika kampuni ya Twiga Minerals Corporation baina yake na Serikali ya Tanzania ni wa ushindi.

 

Akizungumza na waandishi wa Habari kwenye hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro jijini Dar es Salaam, Bw. Bristow amesema, kampuni ya Twiga imepata mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi tangu ianzishwe.

 

Alisema, kabla hata mwaka mmoja haujamalizika tangu kuanzishwa kwake, kampuni ya Twiga Corporation imeweza kujipambanua kuwa na manufaa makubwa na kudhihirisha ushirikiano halisi baina ya kampuni ya uchimbaji madini na Taifa mwenyeji.

Bw. Bristow, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Twiga Corporation, ameonyesha kuridhishwa kwake na ushirikiano huo, ambao amesema umemaliza migogoro ya mara kwa mara iliyokuwa ikijitokeza kati yake na wananchi wanaozunguka migodi.

 

Twiga Minerals Corporation ni kampuni ya ubia baina ya Barrick Gold na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inasimamia na kuendesha amali zote zilizo chini ya Barrick nchini Tanzania, hususan migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara, ikiwemo kutekeleza makubaliano ya pamoja ya kiuchumi.

Pande zote mbili zinagawana faida asilimia 50-50, huku Barrick wakibeba dhamana ya hasara, kama itajitokeza.

 

Kampuni hiyo ilianzishwa mara baada ya Barrick kuchukua uendeshaji wa migodi hiyo iliyokuwa chini ya Acacia Mining mwezi Septemba 2019 na mara moja ikaingia makubaliano na serikali.

 

Katika makubaliano hayo, Barrick inapaswa kulipa Dola za Kimarekani 300 milioni ili kufidia madeni yaliyoachwa na Acacia Mining, yakiwemo ya malimbikizo ya kodi.

Mwezi Mei 2020, Barrick ililipa awamu ya kwanza katika deni hilo, Dola za Kimarekani 100 milioni, lakini Bristow amesema kwamba, mbali ya kulipa kiasi hicho, Barrick pia imelipa zaidi ya Dola 200 milioni kwa serikali kupitia kodi, tozo mbalimbali pamoja na mirabaha, na wiki iliyopita Twiga ilitangaza gawiwo la Dola 250 milioni.

 

“Ukweli kuhusu thamani iliyopatikana katika kipindi hiki kifupi inachangiwa na nguvu ambazo naamini ni ushirikiano wa aina yake barani Afrika. Kwa kuzingatia utekelezaji wa mkataba uliofanyika, tumeweza kumaliza kesi zote za wamiliki wa ardhi (katika migodi yote na hasa North Mara) na sasa tunaelekea kulimaliza tatizo la kimazingira kulingana na vibali vyetu ikiwa ni pamoja na sheria ya kuwashirikisha wenyeji (local content legislation),” alisema.

 

Akaongeza: “Mgodi wa North Mara ambao umeboreshwa umepiga hatua kubwa sana mwaka huu na mgodi wa Bulyanhulu umeanza uchimbaji wa chini ya ardhi (underground mine).

 

“Tumejipanga kuhakikisha migodi ya North Mara na Bulyanhulu inaleta tija kubwa katika awamu ya kwanza, kuhakikisha inazalisha wakia 500,000 za dhahabu kwa mwaka kwa zaidi ya miaka 10 katika nusu ya chini ya viwango vya kampuni (viwango vya asilimia 100).

 

“Tutakuwa tunaangalia uwezekano wa kuongeza uhai wa operesheni zetu sambamba na fursa nyingine nchini Tanzania kwa kuzingatia mfumo wa kampuni ya Twiga.”

Bristow amesema kwamba, Barrick imepatiwa leseni 10 mpya za utafiti nchini Tanzania na inakusudia kutumia Dola 8 milioni katika utafiti mwaka huu.

 

Kujitolea kwa kampuni hiyo katika ushirikiano wa wadau kunahusisha jamii zinazowazunguka na kamati ya maendeleo ya jamii tayari imekwishaanzishwa huko North Mara.

 

Katika upande wa mazingira, mpango madhubuti wa kudhibiti maji (yenye sumu) umekwishaanza kutekelezwa, ambapo tangu Barrick ichukue jukumu la usimamizi mwaka 2019, takriban 50% ya maji yenye sumu katika bwawa huko North Mara yameondolewa.

 

Leave A Reply