The House of Favourite Newspapers

Bayo Na Imbori – 25

0

Kutokana na kiu ya kupata utajiri aliyokuwanayo Bayo ili kurahisisha kazi ya kumtafuta mpenzi wake Imbori anaamua kwenda kwa waganga alioamini wangeweza kumsaidia kufanikiwa hilo.

Kwa mnganga wa kwanza alishindwa masharti aliyopewa, hakukata tamaa akaenda kwa mganga mwingine aitwaye Matiku Ndobori aliyemtaka kumtoa kafara rafiki yake Samson jambo ambalo Bayo alikubaliana nalo baadaye baada ya kuwaza kuwa Imbori alikuwa bora kuliko Samson.

TAMBAA…

KWA mwendo wa taratibu huku akiwa amefunganisha mikono yake nyuma, alianza kupiga hatua kuelekea ulipokuwa mlango wake, alipoufikia alitoa ufunguo mfukoni na kuanza kuufungua lakini ile anakizungusha kitasa mara aliisikia sauti ya mtu jambo lililomfanya ashituke mpaka ufunguo ukadondoka.

“Kaka vipi?” alikuwa ni Jordan akimuuliza.

“Poa tu.”

“Unaonekana hauko sawa!”

“Hapana niko sawa.”

“Si kweli, nimekufuatilia kama siku tatu hivi, kila nikikuangalia nakuona kama kuna jambo kubwa linakutinga.”

“Niamini Jordan niko sawa.”

Jordan alishindwa kulazimisha kuelezwa ukweli na Bayo juu ya nini kilikuwa kinamsibu, lakini kwa kumuangalia tu alifahamu dhahiri hakuwa sawa, jambo aliloamua kulifanya ilikuwa ni kuyaacha ya Ngoswe kuwa ya Ngoswe.

Kwa upande wa Bayo baada ya Jordan kuondoka katika eneo hilo alibaki ameduwaa akishindwa achukue uamuzi gani maana alikuwa anahisi kuelemewa na mzigo mzito wa mawazo aliokuwa ameubeba.

Jambo lililozidi kumchanganya zaidi ni pale alipokuwa anahisi harufu kali kutoka ndani ya chumba chake, funza nazo aliendelea kuziona zikitambaa kila mahali, alijikuta akiamua kuondoka bila hata kuukumbuka ufunguo wake alioudondosha.

Kwa tabu na mawazo mengi siku hiyo nayo ikakatika, ikaingia siku ya sita, siku ambayo iliuzidisha wakati mgumu kwa Bayo.

Kila mahali alipokuwa alihisi harufu kali ya maiti aliyeozea chumbani kwake, aliziona funza zikimfuata nyuma kila alipokwenda, pia kila mara alisikia sauti ya Samson ikimuita kumuomba akamfungulie mlango atoke kumuokoa kwenye kifo kabla ya siku iliyofuata kufika.

“Mungu wangu,” Bayo alijikuta akiongea peke yake huku akiiweka mikono kichwani.

Wakati huo alikuwa maeneo ya Manzese Darajani amekaa, katika eneo hilo lote aliwaona funza wamemzunguka.

“Mkubwa vipi,” Sauti pembeni yake ilisikika.

“Eeeh!”

“Mbona umeshituka?”

“Hapana.”

“Nahisi una tatizo.”

“Sina.”

“Nimekuona unaongea peke yako?”

“Nilikuwa naimba.”

Bayo hakupenda tena kukaa eneo hilo, alifahamu mambo yalikuwa yamekwishaharibika, aliinuka na kuaamua kuelekea nyumbani kwake moyoni  akidhamiria kupambana na wakati huo mgumu aliokuwa anaupitia lakini si kukifungua chumba chake ili aone nini kingetokea atakapoufungua mlango siku iliyofuata.

Sekunde, dakika na saa zilizidi kuyoyoma taratibu mno hatimaye baada ya giza Bayo aliuona mwanga wa jua ukichomoza katika siku ya saba ya mtihani aliopewa na mganga wa kienyeji Matiku Ndobori.

Jambo lililomshangaza na kumfurahisha asubuhi hiyo, hakuziona funza kama ilivyokuwa mwanzo, hakuhisi harufu wala kuisikia sauti ya Samson, mambo yalikuwa shwari kabisa, alipojiridhisha hakukuwa na mtu yeyote nyumbani pale, alikwenda na kukifungua chumba chake.

Hakuamini kile alichokiona, zilikuwa ni pesa zimeenea chumba kizima, alishindwa kuizuia furaha yake akajikuta akipiga kelele mfano wa mwendawazimu huku akijipigapiga kifuani akisema, “ Wagumu tunadumu” kauli iliyomaanisha kujipongeza kutokana na uvumilivu aliokuwa nao hadi kufanikisha zoezi hilo.

 Hakuhitaji kabisa hata nukta itokomee bila kuifikisha taarifa hiyo kwa mganga wake Matiku Ndobori aliyemchukulia kama Mungu wakati huo, alikifunga chumba hicho na kukimbia moja kwa moja hadi nyumbani kwa mganga huyo.

“Yametimia,” aliongea kwa sauti ya juu alipofika kwa Matiku Ndobori.

“Nini?” Matiku alimuuliza.

“Nimekuwa tajiri.”

“Nani kakwambia?”

“Nimeona.”

Matiku alielewa hali ya furaha aliyokuwa nayo Bayo ilitokana na pesa alizoziona chumbani kwake, ilibidi amtulize kisha akampongeza kwa ujasiri aliokuwanao kwa muda wa siku saba,  akampa maelekezo ya kuzitumia kisha akamruhusu aondoke huku moyoni Bayo akipanga kwenda kuianza mara moja kazi ya kumtafuta Imbori.

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply