The House of Favourite Newspapers

Bayo Na Imbori -28

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Dickson anadokezwa na Dk. Frank juu ya uwepo wa Bayo aliyedaiwa kuuawa miaka mitatu iliyopita na Kundi la Kigaidi la Kid Can Kill (KCK), taarifa ambayo ilimchanganya sana akabaki akijiuliza maswali mengi juu ya kuishi kwa mtu aliyefahamu aliuawa bila kupata majibu yoyote yale, alichoamua kufanya ilikuwa kumpa taarifa hizo rafiki yake Richard.Endelea…

“Unaongea ukweli?” Richard alimuuliza.

“Ndiyo, Frank kaniambia.” Dickson alijibu.
“Dah! Tunafanyaje?”
“Richard ninahisi kichwa changu kimefika mwisho kuwaza, haya mambo yamekuwa mengi mno na hakika yamenielemea!”

“Basi hilo niachie mimi, endelea kumtafuta Imbori nitalishughulikia.”
Siku hiyo Dickson alishinda amelala ndani ya chumba cha hoteli aliyofikia na Imbori kutoka Marekani akiwa hana raha hata punje.

Roho yake ilikuwa inamuuma mno, alitokwa na machozi muda wote kama mtoto mdogo, alikuwa anamlilia Imbori, ukweli ni kwamba alimpenda mno, hakutamani kusikia taarifa yoyote ya kuumiza juu ya msichana huyo.

Kila mara alipiga magoti akimuomba Mungu amlinde huko aliko, alitamani utokee muujiza Imbori awe mbele yake katika wakati huo lakini haikuwa inawezekana, Dickson hakuchoka kumtafuta, siku iliyofuata alikuwa tena mitaani na kundi la wanausalama wakimsaka msichana huyo.

Kama mchezo hatimaye siku tatu zilikatika bila Imbori kupatikana, japo kina Dickson walimtafuta kila kona hakukuwa na dalili za kumpata, hali hiyo ilizidi kumuumiza Dickson kiasi kwamba ulifika wakati akakata tamaa ya kumpata mwanamke huyo.

Dickson akawa anatembea mitaani mfano wa mwendawazimu akimuulizia kila mahali lakini bado ikawa kazi bure, si Imbori wala kivuli chake kilichoweza kuonekana, hakujulikana alikuwa wapi na mzima au mfu!
* * *
Msitu wa Keneth Bull ulikuwa ni kati ya misitu maarufu sana Barbados ukisifika kwa kutunza wanyama wakali na viumbe wengine wengi wenye uhai. Mbali na sifa hiyo kwa upande wa kaskazini ulikopakana na Maporomoko ya Jidawi palitumiwa na wakazi wa mji huo wa Briggeton kwa kilimo cha umwagiliaji na ufugaji kutokana na ardhi yake kuwa yenye rutuba ya kutosha.

Mzee Ramson Fent alikuwa ni mmoja kati ya wakulima waliokuwa wanamiliki mashamba makubwa ya mazao ya chakula katika sehemu hiyo, kwa kuwa huo ulikuwa msimu wa mvua kila siku mzee Ramson alilazimika kufika katika Msitu wa Keneth Bull pamoja na vijana wake kwa ajili ya kupalilia na kupanda mazao.

“Baba ona kule,” Robin alimwambia mzee Ramson wakiendelea kulima.
“Kuna nini?”
“Mtu!”
“Amefikaje?”
“Sifahamu.”

“Hebu twende.”
Kwa mwendo wa tahadhari, mzee Ramson alianza kusogea kuelekea kule walikokuwa wamemuona msichana akitembea kwa unyonge huku anapepesuka, wakizidi kumsogelea kabla hata hawajamfikia msichana huyo alianguka chini kama mzigo, jambo hilo liliwashangaza, wakamkimbilia ili waweze kumsaidia.

Walipofika mzee Ramson alimuangalia kwa makini msichana huyo mwenye asili ya Kiafrika, tumbo lake lilikuwa limeingia ndani, akihema kwa kasi huku akiwa ameufumbua mdomo wake.

Mzee Ramson alimtazama kwa makini na kugundua alikuwa na njaa ya muda mrefu, aliamua kumbeba wakarudi naye hadi nyumbani kwake, baada ya kufika walimpa chakula, akala na kushiba baadaye akarudia katika hali yake ya kawaida.

Baada ya kuwa sawa mzee Ramson alimhoji Imbori ilikuwaje mpaka akafika mahali pale, msichana huyo alimuelezea jinsi alivyotekwa na kuterekezwa katika Msitu wa Keneth Bull na watu asiowafahamu.

Zaidi alimuomba mzee huyo kumsaidia afike katika Hoteli ya Good Times alikofikiri angefanikiwa kuonana na Dickson, mzee huyo hakuwa na hiyana alimpeleka Imbori hadi huko akamkabidhi kwa uongozi wa hoteli hiyo ambao walimpa taarifa Dickson kuwa Imbori alipatikana.

“Imbori!” Dickson aliita alipomuona.
“Ni mimi Dickson.”
“Uko hai?”
“Ndiyo.”

“Mungu mkubwa.”
Bila kujali tofauti walizokuwa nazo, Imbori uzalendo ulimshinda, akamkimbilia Dickson na kumkumbatia kwa mikono yake yote huku akibubujikwa machozi ya furaha, moyoni alihisi kuwa mwenye amani kukutana na Dickson, akawa hana uoga tena wa kifo maana alifahamu wakati huo alitua katika mikono salama.

Walipoachiana walielekea mahali tulivu wakaketi na msichana huyo alisimulia kisa kizima cha yaliyotokea baada ya kutekwa hadi kukutana na mzee Ramson aliyemsaidia hadi wakakutana tena.

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

Comments are closed.