The House of Favourite Newspapers

The World You Left Behind 41

Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.

Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.

Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni Mombasa, Kenya ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Grace anasafiri kuelekea Israel kikazi na Magesa anaitumia nafasi hiyo kumpekua mwanamke huyo akitaka kuujua ukweli wa maisha yake. Anachokutana nacho kinamshangaza sana. Hatimaye Grace anarejea na Magesa anambana kwa maswali magumu, hali inayosababisha mwanamke huyo apasue jipu na kueleza ukweli.

Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi na viongozi wa juu wa usalama, wamepeana saa 72 kuhakikisha ukweli unafahamika kuhusu kilichojificha nyuma ya mauaji hayo.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Kama una jambo lolote unalolijua nakuomba uniambie Grace kuliko kuniweka roho juu kiasi hiki.”

“Hapana, hakuna ninachokijua ila najaribu kukuuliza maswali ya hapa na pale ili kukufanya mwenyewe ukishughulishe kichwa chako, huenda majibu mengine unayo wewe mwenyewe,” alisema Grace na kusababisha Magesa azame kwenye dimbwi zito la mawazo.

Kila kitu alichokuwa anaambiwa na Grace kilikuwa kikizidi kukichanganya kichwa chake mpaka akawa anahisi amebeba jiko la mkaa kichwani. Alijaribu kuvuta taswira ya mwanaye Ivan kichwani mwake, akawa anamfananisha na watoto wake wengine, akajikuta akizidi kufika mbali kimawazo.

“Sasa unanisaidiaje Grace? Maana nahisi kama nataka kuchanganyikiwa akili.”
“Kwa nini uchanganyikiwe akili kwa mambo ya ulimwengu uliouacha nyuma yako Magesa?”

“Hata kama ni ulimwengu niliouacha nyuma yangu Grace, roho inauma sana kuanza kugundua mambo kama haya. Hata kama watu wote wanajua kwamba nimekufa ukweli ni kwamba bado nipo hai na naamini siku moja ulimwengu wote niliouacha nyuma yangu utaujua ukweli kwamba sikufa na lazima nilipe kisasi kwa wote waliohusika kuyaharibu maisha yangu,” alisema Magesa huku akionesha kuwa na huzuni kubwa ndani ya moyo wake.

“Pole kama unaumia lakini inabidi uujue ukweli hata kama unakuumiza kiasi gani. Najua umeishi gizani kwa muda mrefu na kuna mambo mengi yalikuwa yakiendelea nyuma ya kisogo chako bila mwenyewe kujua, huu ndiyo wakati wako wa kuujua ukweli na nakuahidi nitakuwa pembeni yako kwa kila kitu,” alisema Grace huku akimpigapiga Magesa mgongoni kama ishara ya kumbembeleza.
* * *
Ephraim Mandiba, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usalama wa Taifa, akishirikiana na vijana wake kadhaa waliokuwa wamebobea katika teknolojia ya mawasiliano sambamba na wataalamu wa sekta hiyo kutoka idara ya mawasiliano ya taifa, waliendelea kufuatilia kwa kina mawasiliano ya marehemu Mwampashi.

“Kuna hizi nyaraka zilitumwa kupitia barua pepe ya marehemu kwenda kwa Magesa, tunaweza kujua ni nyaraka gani na inawezekana kuzipata?”

“Ndiyo, tunaweza kujua ni nyaraka gani na inawezekana pia kuzipata lakini ni lazima tupate moja kati ya laptop au kompyuta zilizotumika kutuma au kupokea.”

“Laptop ya marehemu Mwampashi iliibwa siku ya tukio la ujambazi nyumbani kwake, pia Magesa naye kama mnavyojua amefariki kwa hiyo itakuwa vigumu kidogo kupata laptop yake lakini kama tukielekeza nguvu zetu hapo kwa kuanzia tunaweza kupata mwanga,” alisema Mandiba akiwa na vijana wake sambamba na wale watalaamu wa idara ya mawasiliano, wakiwa ndani ya chumba maalum cha mawasiliano (control room).

Kwa kuwa Mandiba alikuwa na saa 72 tu za kukamilisha kazi hiyo, na tayari saa kadhaa zilikuwa zimeshakatika, hakutaka kuendelea kupoteza muda.

Harakaharaka aliwagawa vijana wake. Wawili wakatumwa kwenda nyumbani kwa marehemu Abbas Magesa kwa ajili ya kufuatilia laptop yake, wawili wakatumwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya kufuatilia namba za usajili wa laptop ya marehemu Mwampashi kwani ofisi yake ilikuwa chini ya wizara hiyo.

Yeye mwenyewe alibaki hapohapo idara ya mawasiliano kwa ajili ya kuendelea kukusanya taarifa nyingine muhimu kuhusu mawasiliano ya Mwampashi na Magesa. Aliendelea kujiuliza maswali mengi ndani ya kichwa chake bila majibu.

Inspekta Jordan Ngai, Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi naye hakuwa na muda wa kupoteza, kwa kushirikiana na vijana wake waliobobea katika masuala ya upelelezi, hasa kutoka vitengo vya CSI (Crime Scene Investigation) na Forensic Investigation alianza kazi mara moja.

Kwa kuwa tayari mezani kwake kulikuwa na ripoti ya awali iliyoonesha kwamba maganda ya risasi yaliyookotwa eneo la tukio, nyumbani kwa CAG Mwampashi yalikuwa na namba zinazoonesha kwamba bunduki zilizotumika zilikuwa zimesajiliwa kwa usajili wa serikali, kazi ilianzia hapo.

Inspekta Ngai aliwapanga vijana wake, wakiwemo wale walioshughulikia kupatikana kwa ile ripoti ya mwanzo na akawasisitiza kuhakikisha kila kitu kinachunguzwa kwa kina ili kupata majibu ya uhakika.
“Bila shaka wewe ndiyo Dokta Mathias Msalala.”
“Ndiyo mkuu.”

“Wewe ndiye uliyeufanyia vipimo mwili wa marehemu Daniel Mwampashi, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.”
“Ndiyo mkuu.”

“Ripoti yako ya uchunguzi ulimkabidhi nani?”
“Nilimkabidhi mkuu wa idara yangu na nakala moja niliiweka kwenye faili kama utaratibu wa kazi unavyoniagiza.”
“Ukiiona ripoti yako unaweza kuitambua?”

“Mkuu, nitashindwaje kukitambua kitu nilichokiandika mwenyewe?”
“Hebu itazame, ni hii?” alisema Ngai huku akitoa ripoti ya uchunguzi wa mwili baada ya kifo (Post Mortem) kwenye briefcase yake na kumpa Dokta Mathias Msalala.
“Hapana, hii sikuiandika mimi.”

“Hii iliandikwa na nani? Na kama hukuandika wewe mbona hapa chini kuna jina lako na sahihi yako?”

“Mkuu, niamini ninachokwambia. Hata sielewi nini kilichotokea lakini hii siyo ripoti niliyoiandika mimi,” alisema daktari huyo huku na yeye akionesha kushangazwa sana na maelezo hayo. Akaandika maelezo kwenye kitabu chake cha kumbukumbu na kuendelea kumhoji daktari huyo ambaye tayari hofu kubwa ilishaanza kumuingia.

“Unakumbuka mwili wa marehemu ulipoletwa ulikuwa na hali gani?”
“Ulikuwa na matundu mengi ya risasi, hasa kifuani upande wa kushoto na kichwani.”
“Ulitoa risasi ngapi ndani ya mwili wake?”

“Risasi tisa ambazo zilikuwa na ukubwa tofauti kuonesha kwamba bunduki mbili tofauti zilitumika.”
“Ziko wapi hizo risasi?”

“Kwa kawaida huwa tunawakabidhi polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwa hiyo na mimi niliwakabidhi baada ya kumaliza kazi yangu.”
“Unakumbuka ulimkabidhi nani?”

“Siwezi kumkumbuka kwa jina lakini kwa sababu katika makabidhiano ya aina hiyo ni lazima tujaze kitabu maalum cha ‘dispatch’, ngoja niangalie jina lake anaitwa nani,” alisema daktari huyo huku kijasho chembamba kikimtoka. Harakaharaka akafungua kabati linalotumika kuhifadhia mafaili na vitabu vingine vya kumbukumbu.

Alifanikiwa kukipata kitabu hicho lakini katika hali iliyomshangaza kila mmoja, ukurasa ambao ndiyo daktari huyo aliodai kwamba alijaza taarifa hizo, ulikuwa umechanwa.
“Kwani ofisi hii mnatumia watu wangapi?”

“Tunatumia wengi mkuu lakini hakuna mwenye tabia ya kupekua vitu visivyomhusu.”
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne ijayo kwenye gazeti hilihili.

Comments are closed.