The House of Favourite Newspapers

Bayo Na Imbori -31

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Baada ya Imbori kuteseka muda mrefu hospitali kwa kukosa mtu wa kumtolea figo hatimaye anapatikana kijana kutoka Tanzania, Bayo aliyefanya mawasiliano na Dickson kupitia namba ya simu iliyokuwa imewekwa kwenye mtandao wa www.gospcopp.com akatakiwa kwenda Marekani kwa ajili ya zoezi hilo.Tambaa Nayo…

BAYO alionekana kuwa mkombozi kwenye maisha ya Imbori, baada ya kufika Marekani na kufanyiwa vipimo sifa za afya na figo yake vilitosha kabisa kumchangia figo msichana huyo, lakini kabla ya kufanyiwa upasuaji wa figo, Bayo alihitaji kumuona kwanza Imbori suala ambalo hakuna aliyelipinga.

“Imbori!” Bayo aliita akimtazama kwa masikitiko.
Imbori ambaye tangu azidiwe hakuwa na uwezo wa kuongea alifungua macho na kutazama ni nani aliyeliita jina lake. Kwa tabu macho yake yakangongana na ya Bayo, upande fulani wa kumbukumbu kwenye ubongo ukamwambia huyo aliyekuwa anamuona mbele yake alikuwa ni Bayo kijana waliyekuwa wanapendana mno, hakuna aliyefahamu msichana huyo alizitoa wapi nguvu hadi kusimama na kukumbatiana na Bayo!

“Mambo vipi mpenzi?” Bayo aliongea huku machozi yanambubujika.
“Poa!”

“Mbona uko katika hali hii!”
“Ni Dickson!”
“Amefanya nini!”
“Ndiye aliyesababisha haya yote!”
“Kivipi?”

“Si alitutenganisha!”
Wakati wakiwa bado wamekumbatiana Imbori aliishiwa nguvu, akalegea na kuponyoka mikononi mwa Bayo kisha akadondoka chini kama mzigo. Si Dk. Mand wala Dickson aliyekuwa anaamini kile walichokuwa wanakiona mbele yao, ilikuwa ni mfano wa tamthiliya fulani ya kusisimua walikuwa wanaitazama kwenye televisheni.

Bila kuongea neno lolote, Dickson na Dk. Mand walisaidiana na Bayo kumbeba Imbori na kumweka kwenye kitanda cha wagonjwa kisha daktari huyo pamoja na manesi wawili waliokuwepo wakampa huduma ya kwanza Imbori. Baada ya hapo walimtaka kupumzika pia Bayo alitolewa kwenye chumba hicho cha wodi.

***
“Lazima kuna jambo tunatakiwa kufanya!” Dickson alimwambia Dk. Mand.
“Jambo gani?”
“Kuua.”

“Kumuua nani na kwa nini?”
“Bayo, kwa sababu kuwepo kwake kunamaanisha kumkosa Imbori.”
“Haiwezekani, tukimuua nani atatoa figo?”
“Atapatikana mwingine!”
“Wapi?”

“Kokote duniani.”
“Hata hivyo kuua mimi siwezi.”
“Unaweza ni rahisi sana.”
“Hapana siwezi.”

“Dokta nitakulipa kiasi chochote cha pesa unachotaka.”
“Ni kinyume na maadili ya kazi yangu.”
“Wakati huu hatuzungumzii maadili na weledi kwenye kazi ni kukubali kuua upate pesa dokta.”

Ilikuwa kazi ngumu kwa Dickson kumshawishi Dk. Mand kukubali kumuua Bayo baada ya kumfanyia upasuaji wa figo lakini kutokana na ushawishi wa fedha aliokuwa nao, dokta huyo hakuweza kuruka. Bila kulazimishwa alikubaliana na jambo hilo lakini kwa masharti ya kulitekeleza baada ya Imbori kupata unafuu ili wasije wakaharibu mambo mawili kwa wakati mmoja, Dickson hakuwa mbishi.

Kulipopambazuka katika siku iliyofuata, Bayo alifanyiwa vipimo kwa mara nyingine kuangaliwa presha yake ya damu kama ilikuwa inaruhusu upasuaji ufanyike au la, alipoonekana kuwa sawa alipelekwa kwenye chumba cha upasuaji akaondolewa figo moja aliyokwenda kuwekewa Imbori.

Baada ya wiki moja tangu Imbori abadilishiwe figo alionekana kuwa na nafuu kwa kiasi kikubwa. Hapo ndipo mipango ya kumuua Bayo ilipoanza, Dickson alimshawishi Dk. Mand amuue kwa kumchanganyia sumu kwenye chakula ambacho angepewa kama ulivyokuwa utaratibu wa kila siku kumhudumia Bayo. Chakula alichoambiwa kilikuwa msaada mkubwa kwake kiafya baada ya kufanyiwa upasuaji wa figo.

***
Jopo la wapelelezi lililokuwa linaongozwa na kamanda James Mansion lilikuwa kazini likiendelea na uchunguzi dhidi ya watu waliohusika kumpiga risasi Imbori. Kama lilivyokuwa azimio lao walilichukua faili lililoonesha majina ya wahudhuriaji wote waliofika kwenye Ukumbi wa MGM Grand Gorden kushuhudia Mashindano ya Usaili wa American Idol kisha wakaanza kuyapitia majina moja baada ya lingine.
Kazi hiyo ilifanyika kwa uangalifu mkubwa, malengo ya James Mansion na wenzake yakiwa kuutafuta mwanzo ambao ungewasaidia katika uchunguzi wao, ambapo kutokana na maelezo ya Dickson ilionekana watu waliokuwa wanamfuatilia Imbori walikuwa ni watu wake wa karibu ambao alikuwa amekwaruzana nao.
Je, nini kitaendelea? Imbori atapona? Mipango ya kumuua Bayo itafanikiwa? Usikose wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply