The House of Favourite Newspapers

Bayo Na Imbori -31

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Kabla ya Imbori kuzidiwa na kuhitaji figo, alimtaka Dickson aliyekuwa ameanzisha naye uhusiano wa mapenzi kumtafutia shule ya muziki ili akakinoe zaidi kipaji chake cha uimbaji alichokuwa nacho, jambo ambalo Dickson hakuweza kulipinga!

Tambaa nayo…
KAMA alivyohitaji Imbori, asubuhi ya siku iliyofuata Dickson alimpeleka katika Chuo cha Marvin Music Techniques alikomwandikisha kuchukua kozi ya miezi sita ya kujifunza mpangilio wa sauti na ala za muziki.

Siku chache zilizofuata Imbori alikuwa amekwishaanza masomo na alitokea kuwa kivutio kikubwa kwa wanafunzi wengi na walimu, kwanza kutokana na uzuri wake lakini pili uwezo wake mkubwa wa kuimba na kutumia ala za muziki.

Siku zikazidi kusonga mbele huku Imbori akizifurahia mali na penzi la Dickson pia umaarufu wake Marekani ulianza kupaa taratibu kutokana na sifa ya uwezo wake wa kuimba kuanza kusambaa kwa kasi. Watu wengi wakawa wanahitaji kumfahamu lakini baadaye alikuja kufahamika zaidi baada ya kujitosa kwenye mashindano ya uimbaji ya American Idol.

* * *
Hiyo ilikuwa siku tulivu ambayo Imbori alitakiwa kupanda jukwaani katika awamu ya nne ya Usaili wa Mashindano ya American Idol kuimba wimbo wa Imposible ulioimbwa na mwanadada mrembo aliyezaliwa nchini Barbados, Shontelle Layne ‘Shontelle’ na kuuachia Februari 9, 2010.

Umati mkubwa wa watu, mbali na wale waliokuwa wanafuatilia majumbani kupitia televisheni, ulikuwa umejaa katika Ukumbi wa MGM Grand Garden Arena uliopo kusini mwa mji wa Las Vegas huko Nevada wakimsubiri kwa hamu msichana huyo. Miongoni mwa watu hao alikuwa Josephine na vijana wawili waliovaa miwani, aliokuwa anawatumia msichana huyo katika mpango wa kumuua Imbori baada ya mbinu zake za mwanzo kushindikana.

Japo washiriki mbalimbali waliendelea kufanya vitu vyao jukwaani, ukweli ni kwamba shauku ya watu wengi ilikuwa kumuona Imbori aliyevuma ghafla kama upepo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuimba.

“Ladies and gentlemen the next contestant is…scream… for …Imboriiiiiiii” (Mabibi na Mabwana mshiriki anayefuata ni…piga… kelele… kwa ….Imboriiii)

Baada ya sauti hiyo ya mshereheshaji wa siku hiyo ambaye ni mchekeshaji maarufu Marekani, Kelvin Hart, ukumbi mzima ulilipuka kwa shangwe na wakati huohuo DJ Q, alipenyeza wimbo wa Impossible. Sauti tamu ikaanza kusikika ikizipandilia kick, snea na piano zake, kisha akaanza kuonekana msichana mrembo akiingia kwa pozi jukwaani.

I remember years ago
Someone told me I should take
Caution when it comes to love
I did, I did
And you were strong and I was not
My illusion, my mistake
I was careless, I forgot
I did

And now when all is done
There is nothing to say
You have gone and so effortlessly
You have won
You can go ahead tell them….

Ukumbi mzima ulikuwa kimya, watu wakisikiliza kwa makini namna ambavyo sauti tamu ya msichana Imbori ilivyokuwa ina kita kwenye spika zilizozunguka kila mahali ukumbini hapo, wengine walikuwa wanafuta machozi kutokana na hisia ya furaha kuwazidia. Wakati Imbori akiendelea kulishambulia jukwaa, risasi zikarindima.

PA! PAA! PAAA!
Ghafla sauti iliyokuwa inasikika kwenye spika ikakata, Imbori akadondoka kama mzigo jukwaani, kila mmoja akaanza kukimbia kuelekea nje ili aokoe maisha yake. Dickson pekee ndiye aliyemudu kukimbia hadi pale alipokuwa amedondokea Imbori huku akilia kwa uchungu.

Ukweli ni kwamba kijana huyo hakupenda kabisa kuamini kile alichokuwa anakiona mbele yake, Imbori alikuwa katikati ya dimbwi la damu. Kwa namna yoyote alionekana hakuwa na hata chembe moja ya uhai, Dickson alifikiri alikwishafariki dunia.

“Please, Imbori don’t die, it’s too early to leave me alone,” (Tafadhali Imbori usife ni mapema sana kuniacha mpweke), Dickson alitamka kwa nguvu huku akishindwa kumudu kuzizuia hisia zake, aliendelea kulia mfululizo huku akimpigapiga Imbori.

Wakati huo eneo hilo lote la ukumbi lilishakuwa kimya, watu wote walikimbilia nje lakini baada ya dakika chache waliingia watu watatu wenye miili ya miraba minne waliovaa mavazi yenye kuwatambulisha kuwa ni walinzi wa hotelini hapo.

Walisaidiana na Dickson wakambeba Imbori na kumtoa nje kisha wakamweka kwenye gari aina ya Marcedes Benz, safari ya kuelekea kwenye Hospitali ya White Heart iliyoko kilometa nane kutoka katika ukumbi huo wa MGM Grand Arena ikaanza mara moja. Dakika 10 baadaye walikuwa wamekwishafika.

Je, nini kitaendelea? Nini kilitokea mpaka Imbori akatakiwa kufanyiwa upasuaji wa Figo? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply