The House of Favourite Newspapers

Benki ya NBC, Taasisi ya Benjamini Mkapa Wazindua Ufadhili wa Mafunzo ya Ukunga kwa Wauguzi 50

0
Baadhi ya wanafunzi wanufaika wa mpango wa ufadhili wa masomo ya ukunga kwa wauguzi 100 unaofadhiliwa na benki ya NBC kupitia taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation (nyuma waliosimama) wakionesha mikataba ya ufadhili wakati wakati uzinduzi wa utekelezaji wa mpango huo uliofanyika katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi  Morogoro leo.  Uzinduzi huo uliongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio (Katikati walioketi). Wengine ni pamoja na Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano wa benki ya NBC Bw Godwin Semunyu, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, Dkt Ellen Mkondya Senkoro (wa pili kushoto) na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi  Morogoro Dkt Damas Missanga (wa pili kulia).

Morogoro, Benki ya NBC kwa kushirikaina na taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation wamezidua rasmi utekelezaji wa mpango wa ufadhili wa masomo ya ukunga kwa wauguzi 50 kati ya 100 wanaonufaika na mpango huo ikiwa ni muendelezo wa jitihada za wadau hao wawili katika kukabiliana na changamoto ya vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Mpango huo unaofahamika kama Mkapa Fellows Scholarship Program unahusisha ufadhili wa kiasi cha sh. Milioni 211 kutoka benki ya NBC ukilenga  kuongeza ujuzi  kwa wauguzi 100 katika ngazi ya diploma ya ukunga ya mwaka mmoja, katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi  Morogoro. Fedha hizo ni sehemu fedha iliyokusanywa na benki hiyo kupitia mbio yake ya hisani inayofahamika kama ‘NBC Dodoma Marathon; iliyofanyika mwezi Julai mwaka huu jijini Dodoma.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio (Kulia walioketi) sambamba na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, Dkt Ellen Mkondya Senkoro wakisaini hati ya makubaliano ya kiutendaji katika utekelezaji wa mpango wa ufadhili wa masomo ya ukunga kwa wauguzi 100 unaofadhiliwa na benki ya NBC kupitia taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation wakati wakati uzinduzi wa utekelezaji wa mpango huo uliofanyika katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi  Morogoro leo.  Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano wa benki ya NBC Bw Godwin Semunyu (katikati waliosimama), Kaimu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi  Morogoro Dkt Damas Missanga (wa pili kulia waliosimama) pamoja na maofisawengine waandamizi wa benki ya NBC na ofisi ya Mganga Mkuu mkoa wa Morogoro.

Uzinduzi huo umefanyika leo chuoni hapo ukihusisha zoezi la utiaji saini makubaliano ya mpango huo baina ya wadau hao ikiwemo taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation, Serikali kupitia Mganga Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi  Morogoro na wanafunzi hao. Utiaji saini huo ni mwendelezo kufuatia zoezi kama hilo lililofanyika mwezi Julai mwaka huu likihusisha wadau wakuu wa mpango huo ambao ni benki ya NBC na taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation.

Akizungumzia hatua hiyo Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano wa benki ya NBC Bw Godwin Semunyu aliemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, alisema inalenga kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini hususani katika kukabiliana na matukio ya vifo vya wakina mama na watoto wakati wa kujifungua.

“Kama taasisi mwajibaki kwa jamii tunayoihudumia, Benki ya NBC tunatambua uharaka wa kukabiliana na vifo vifo vitokanavyo na changamoto mbalimbali za uzazi hapa nchini. Tunaamini kwamba kwa kuwekeza katika elimu na mafunzo ya wakunga wauguzi, tunaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha na kuboresha matokeo ya huduma za afya kwa akina mama na watoto wachanga.’’ Alisema Semunyu.

Hatua ya benki hiyo inakuja wakati ambapo Tanzania licha ya jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na serikali bado inakabiliwa na changamoto katika upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wajawazito, hali inayopelekea vifo vingi vya wakina mama na watoto wakati wa kujifungua. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2020, karibu asilimia 95% ya vifo vyote vya uzazi vilitokea katika nchi zinazoendelea, huku viwango vya vifo vya wajawazito nchini Tanzania (MMRs) vikiwa karibu 500 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, Dkt Ellen Mkondya Senkoro  (alieketi) akiwashuhudia wanafunzi mbalimbali wanufaika wa mpango huo wakisaini hati ya makubaliano ya kiutendaji katika utekelezaji wa mpango wa ufadhili wa masomo ya ukunga

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, Dkt Ellen Mkondya Senkoro alisema kupitia mpango huo, wauguzi walioandikishwa kutoka vituo vya afya vya umma watapata fursa ya kupandishwa hadhi na kufikia kiwango cha diploma ya uuguzi (majors in midwifery).

“Wakunga hawa wauguzi wanawezeshwa ili kuongeza ujuzi na utaalamu wao ili kuboresha ubora wa huduma kwa mama wajawazito na kupunguza hatari ya vifo vya uzazi. Tunaamini katika upatikanaji sawa wa huduma bora za afya kwa wote. Hivyo kupitia mpango huu wa ufadhili wa masomo, tunaongeza wigo wa kufikia  jamii ambazo hazijahudumiwa na kuboresha  uzazi salama. Matokeo ya kuboresha huduma hizi yatapelekea kuwa na mama na watoto wachanga wenye afya njema…kwa hili tunawashukuru sana wenzetu benki ya NBC’’. Alisema.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio (Katikati mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na maofisa wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation wakiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt Ellen Mkondya Senkoro ( kushoto kwake), maofisa wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano wa benki ya NBC Bw Godwin Semunyu (kulia kwake) uongozi na wakufunzi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi  Morogoro wakiongozwa na Kaimu Mkuu wa chuo hicho Dkt Damas Missanga (wa saba kushoto) pamoja na wanafunzi wanufaika wa mpango wa ufadhili wa masomo ya ukunga kwa wauguzi 100 unaofadhiliwa na benki ya NBC kupitia taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation wakati wakati uzinduzi wa utekelezaji wa mpango huo uliofanyika katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi  Morogoro leo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio alisema licha ya jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na serikali katika kukabiliana na vifo vya kina mama na watoto wakati wa kujifungua, bado kuna changamoto kadhaa zinazokwamisha jitihada hizo ikiwemo wakunga wengi kutokuwa na uwezo wa kutosha kukabiliana na dharura zinazoibuka wakati wa kujifungua.

Alitaja sababu nyingine zinazasababisha vifo hivyo  ni pamoja na wakunga kushindwa kutibu watoto wanaozaliwa wakiwa na changamoto zinazohitaji matibabu ya haraka pamoja na baadhi ya wakunga kushindwa kuzingatia ‘partographs’ za wajawazito hatua inayopelekea wengi wao kushindwa kutambua vema mwenendo wa afya ya mtoto akiwa tumboni ili kujua tahadhari inayohitajika kuchukuliwa kabla ya wakati wa kujifungua mwa wanawake husika.

“Hata hivyo zipo jitihada kadhaa ambazo tunachukua kama serikali hususani hapa mkoani Morogoro ambapo tunahakikisha tunawajengea uwezo zaidi wakunga kupitia mipango yetu kama serikali na kushirikiana na wadau kama hivi. Zaidi pia tunahakikisha kila hoispitali ya wilaya inakuwa na timu ya wataalamu wa kutosha na weledi mkubwa katika  kushughulikia dharura mbalimbali za uzazi…na ndio sababu tunawasisitiza sana wakunga wakiona kuna changamoto inawazidi uwezo watoe rufaa haraka ili kuokoa maisha ya mama na mtoto ,’’ alisema.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi  Morogoro Dkt Damas Missanga aliwataka wanafunzi hao kutumia vema ufadhili huo kwa kuzingatia mafunzo mbalimbali yanayotolewa chuoni hapo huku akikisisitiza utayari wa wakufunzi na uongozi wa chuo hicho katika kuhakikisha waanafunzi hao wanahitimu kwa ustadi wa hali ya juu ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa kupitia mpango huo.

Kwa upande wao baadhi ya wanufaika wa mpango huo Yusuph Chinguile, Angelina Amosi na Simon Bundala pamoja na kuwashukuru wafadhili wa mpango huo walisema kupitia mafunzo hayo yaliyoanza tangu katikati ya mwezi Oktoba wanajifunza kushughulikia na uzazi wenye changamoto hatua ambayo ni muhimu zaidi ikilinganishwa na hapo awali ambapo elimu waliyokuwa nayo ni kushughulika na uzazi usio na changamoto.

“Wengi wetu tumekuja hapa kama ambavyo ilivyo kwa wengi ambao hawajapata nafasi hii tulikuwa hatuna ujuzi wa kutosha kushughulikia changamoto zisizo za kawaida zinazojitokeza wakati wa kujifungua. Ujuzi tuliokuwa nao awali ni kushughulikia uzazi wa kawaida usio na changamoto. Na hii ndio sababu wengi wetu tunajikuta tunashindwa kuokoa maisha ya mama na mtoto ikitokea changamoto kubwa na wataalamu hawapo karibu…kwa hiyo tunawashukuru sana NBC na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation kwa ujio wa mpango huu,’’ alisema Muuguzi Simon Bundala.

Leave A Reply