The House of Favourite Newspapers

Benki ya NMB yapunguza riba za mikopo kutoka 19% hadi 17%

Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker (kulia) akizungumza jambo.
Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker, Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Higher Education Students’ Loans Board, Phidelis  Joseph na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Utoaji Mikopo, Sara Fihavango.
Mkuu wa Idara ya Wateja wadogo na wa kati kutoka Benki ya NMB, Abdulmajid Nsekela (katikati) akitoa ufafanuzi juu ya ushirikiano huo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Wakishikana mkono kama ishara ya ushirikiano baina ya Benki ya NMB na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Higher Education Students’ Loans Board).

BENKI ya NMB imepunguza kiwango cha riba katika mikopo yake kwa wateja kutoka asilimia 19 hadi 17 kwa wateja wanaokopa kupitia mishahara kwa waajiriwa wa mashirika ya umma na wale wa binafsi.

 

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Bi. Ineke Bussemaker amesema benki hiyo imechukua hatua hiyo ikiwa ni utaratibu kupunguza riba kwa wateja wake.

 

Alisema punguzo hilo limegusa viwango vyote vya mikopo kwa kutumia mishahara kutoka kiwango cha chini cha shilingi 200,000 hadi cha juu cha shilingi milioni 150 kutegemea mshahara wa mkopaji.

 

Aliongeza kuwa ili kujenga mazingira mazuri kwa wateja wao mikopo yao sasa inashughulikiwa ndani ya  saa 24 hadi muhusika anapokea mkopo wake.

 

“Wateja wetu wengi wa mikopo wamekuwa wakiomba tupunguze riba za mikopo yetu jambo ambalo tumelizingatia kwa sasa na tumeongeza ofa ya gharama bure za kushughulikia mikopo hiyo kwa wiki sita kuanzia leo,” alisema Bi. Bussemaker.

 

Alifafanua kuwa  NMB inasikiliza zaidi ushauri wa wateja wake na ndio maana sasa wameongeza muda wa marejesho ya mikopo kutoka kiwango cha chini cha miezi 60 hadi miezi 72 (sawa na miaka mitano hadi sita).

 

Ongezeko hilo la muda wa kulipa marejesho linaweza kuwanufaisha pia wadaiwa wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ambapo mkopaji anaweza kuzungumza na benki kisha ikalipa mkopo wote naye akaendelea kulipa taratibu kwa mujibu wa makubaliano na benki hiyo.

 

 

Comments are closed.