The House of Favourite Newspapers

Bibi Titi: Mwanamke wa kwanza kupanda jukwaa la kisiasa

0

CEEPvU2UkAAEPXm.jpg large

Bibi Titi Mohammed

Na Elvan Stambuli

Niliwahi kuomba kufanya mahojiano na Bibi Titi Mohammed mwaka 1995 nyumbani kwake, Upanga, Dar. Nikaonana naye na kumfahamisha kuwa nilikuwa nataka kuandika kuhusu harakati zake za kudai uhuru.

Baada ya kumjuza hilo, aliniambia kuwa hazina yake ya nyaraka za wakati wa kudai uhuru pamoja na picha zake nyingi za kihistoria, zilichukuliwa na askari wapelelezi wakati walipokuja kufanya upekuzi katika nyumba yake kutokana na tuhuma za kupindua serikali zilizokuwa zimemkabili katika miaka ya 1970.

Bibi Titi akaniambia kwa siku ile haingewezekana kwa sababu alikuwa anaumwa, akaniomba nimtafute akipona, sikuonana naye tena mpaka alipofariki dunia, Dar, mwaka 2000.

Kwa wale ambao walikuwa karibu na Bibi Titi, watakuwa wanajua jinsi alivyokuwa hodari wa kuzungumza na kushinikiza hoja zake! Ndivyo alivyoikatiza shauku yangu ya kumhoji, nikanywa soda, tukaagana.BibiTitinaMwalimu

Bibi TIti na Mwalimu julius .K .Nyerere

Awali nilidhani kuwa Bibi Titi aliingizwa katika Chama cha Tanganyika African National Union (Tanu) na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kitu ambacho siyo kweli kwani alipohutubia mkutano wa kwanza wa kisiasa jukwaani Juni, 1955, Nyerere alikuwa bado hajajiunga na siasa.

Bibi Titi alijiunga na Tanu mara baada ya kuzaliwa mwaka 1954 na kupewa kadi namba 16 na mumewe, Boi Selemani akapewa kadi namba 15 na wote waliingizwa Tanu na mtu aliyeitwa Schneider Plantan (tutaeleza habari zake matoleo yajayo ya gazeti hili).

Bibi Titi Mohamed alihutubia mkutano wake huo wa mwanzo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, wakati huo Mwalimu Nyerere alikuwa hafahamiki na watu wengi wa Dar es Salaam au nchini.

Uwanja huo kwa jumla, mambo mengi ya watu wa Dar yalikuwa yakifanyika pale. Haikustaajabisha basi kuwa watu wa Dar walifanyia mikutano ya mwanzo ya Tanu uwanjani hapo.

Ni katika uwanja huu ndipo Bibi Titi alipoanza kuwahamasisha Watanganyika wajipinde kuung’oa ukoloni katika ardhi yao. Katika mkutano huo, aliombwa aanzishe tawi la wanawake wa Tanu kwa sababu ya tabia yake ya ucheshi na kupenda kuchanganyikana na watu na hatimaye akawa ndiyo chanzo cha Umoja wa Wanawake wa Tanganyika (UWT) uliokuja kuundwa mwaka 1962, akachaguliwa kuwa mwenyekiti wake wa kwanza.

Alibunije mtindo wa kuwapandisha wasanii jukwaani? Alitumia vikundi gani? Kuyajua yote hayo, usikose kufuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply