The House of Favourite Newspapers

Mawaziri 11 watekwa na magaidi

0

Hebu vuta picha! Mawaziri kibao kutoka nchi mbalimbali duniani pamoja na wadau wengine, wapo kwenye mkutano muhimu wakijadiliana kuhusu mambo muhimu ya kimaendeleo.

Wakiwa wanaendelea na mkutano, ghafla milio ya risasi inaanza kurindima kila kona, watu waliovaa kininja wanaingia wakiwa na silaha nzito na ukumbi wa mikutano unawekwa chini ya ulinzi!  Ni vigumu kutokea si ndiyo?
Basi kwa taarifa yako tukio kama hilo limewahi kutokea. Ilikuwaje? Desemba 21, 1975 mawaziri wa nchi mbalimbali zinazozalisha mafuta (OPEC), walikutana Vienna nchini Austria kujadiliana kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu biashara ya mafuta duniani.

Wakiwa wanaendelea na mkutano, ghafla watu sita waliovalia mavazi ya kuficha nyuso zao, mikononi wakiwa na silaha nzitonzito, walivamia ukumbi huo na ‘kukinukisha’.

Katika majibizano ya risasi, watu watatu walipoteza maisha papo hapo akiwemo polisi mmoja wa Austria, mjumbe kutoka Iraq na mwingine kutoka Libya na kuwateka wengine 96 waliokuwa ndani ya jengo hilo, wakiwemo mawaziri 11 kutoka nchi mbalimbali wanachama wa OPEC.

Magaidi hao walikuwa wakiongozwa na Ilich Ramirez Sánchez ‘Carlos the Jackal’ (pichani), wakiwa bado ndani ya jengo la makao makuu ya OPEC kulipofanyika utekaji, walianza kuishinikiza serikali ya Austria kuviamuru vyombo vyake vya habari kutangaza ujumbe wa kulaani vikali ukandamizwaji uliokuwa ukifanywa na Israel dhidi ya Wapalestina vinginevyo kila baada ya dakika 15, mateka mmoja atakuwa anauawa.

Serikali ya Austria ilikubali, ujumbe ukaanza kurushwa kila baada ya saa mbili kupita. Baadaye, watu 50, raia wa Austria waliokuwa miongoni mwa mateka hao, waliachiwa huru.

Kesho yake asubuhi, Desemba 22, mwaka huohuo, serikali ilitii matakwa mengine ya watekaji hao ya kuwapatia ndege kubwa kwa ajili ya kuwasafirisha magaidi pamoja na mateka 42 kuelekea Algiers.

Watekaji hao wakaondoka mpaka Algiers ambapo baada ya kutua uwanja wa ndege kibabe, serikali ya nchi hiyo ilianza kufanya nao mazungumzo ambapo baada ya kukubaliana baadhi ya mambo, ikiwa ni pamoja na kupewa fedha nyingi kama fidia, mawaziri watano waliachiwa huru pamoja na mateka wengine 31.

Baada ya hapo, watekaji waliomba ndege nyingine ambaye iliwasafirisha mpaka Tripoli, Libya ambako mateka wengine kadhaa waliachiwa huru kwa masharti magumu, ikiwemo ya kutowafungulia mashtaka magaidi hao.

Baadaye walirejea tena Algiers ambako walimalizia kuwaachia mateka wote baada ya kuhakikishiwa kwamba hawatafunguliwa mashtaka. Miongoni mwa watekaji hao, ni mwanamke mmoja tu raia Ujerumani, Gabriele Kröcher-Tiedemann ndiye aliyekamatwa na kusomewa mashtaka.

Leave A Reply