The House of Favourite Newspapers

Binti Akiri Kudanganya Kubakwa, Mtuhumiwa Afungwa Jela Miaka 60

0

BINTI Maria Sanga (20), mkazi wa kijiji cha Kilingi Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, ameamua kuiangukia Serikali kutengua hukumu kwa kijana aliyemsingizia kuwa alimbaka na kumpa ujauzito mwaka 2017.

 

 

Kijana huyo alikuwa kidato cha nne huku yeye akiwa kidato cha pili, na baada ya kesi kusikilizwa mwaka 2018 katika kesi namba moja ya mwaka 2017, Tumaini Frank hatimaye alikutwa na hatia ya kumpa ujauzito Maria na kisha kufungwa gerezani miaka 60.

 

 

Asimulia ilivyokuwa

Akielezea mkasa wa tukio hilo jana mbele ya wanahabari, binti huyo alisema kuwa mwaka 2017 wakati akiwa kidato cha pili, alirudi nyumbani baada ya kumaliza mitihani, wazazi wake wakamshuku kuwa na ujauzito.

 

 

“Mwaka 2017 nilipata ujauzito nikiwa kidato cha pili, mara baada ya kumaliza mitihani yangu, nilirudi nyumbani baada ya kukaa nyumbani wazazi wangu waligundua ni mjamzito. Waliniuliza ujauzito ni wa nani sikuwaambia, wenyewe wakafanya upelelezi wao wakaniambia Tumaini ndiye aliyekupa ujauzito, wakanitishia kunipiga ikabidi niseme,’’ anaeleza.

 

 

“Baada ya kukiri waliyotaka niseme Tumaini alikamatwa na kupelekwa polisi, baadaye niliitwa polisi kwenda kutoa maelezo. Niliandika maelezo yangu na kurudi nyumbani na baadaye kesi ilipelekwa mahakama ya wilaya ya Siha na baadaye nikawa nahudhuria mahakamani ndani ya mwaka mmoja,”alieleza binti huyo.

 

 

“Nakumbuka mwaka 2018 Agosti Tumain alihukumiwa kwenda jela miaka 60. Kwa kweli niliumia sana licha ya kwamba nilikuwa naujua ukweli kwamba sio yeye anahusika na mimba yangu. Nafsi yangu iliendelea kunishtaki ikanilazimu niende ofisi mbalimbali kusema sio yeye aliyenipa ujauzito,”

 

 

“Nilienda ofisi ya kijiji ofisi ya wanasheria Sanya Juu, walinipokea na kuniandika maelezo yangu kuhusu kukataa kwamba hukumu ile hakustahili Tumaini kutokana na kwamba sio yeye alihusika na ujauzito wangu.’’

 

 

Anaendelea; “Nimeona niliseme hili kwa kuwa linaniumiza na huyu anateseka kwa kifungo ambacho sio chake. Ninaziomba mamlaka zinazohusika zinisaidie kwa sababu nililazimishwa na wazazi wangu kumtaja ambaye hahusiki na kipindi hicho bado nilikuwa sina akili za utu uzima.

 

 

Kauli ya baba wa aliyehukumiwa

Baba wa Tumaini, Frank Mfinanga alieleza kuwa tukio hilo lilimuumiza na alilipokea kwa machungu kutokana na mwanawe kuhukumiwa kwa kusingiziwa.

 

 

“Niliumia sana mtoto wangu alipobambikiziwa kesi ya kumpa mimba mwanafunzi mwenzake. Huyu binti ni wa jirani yangu kabisa, kweli hili suala nilipokea kwa machungu na liliniumiza sana baada ya kesi kwenda mahakamani”

 

 

“Baada ya kesi kwenda mahakamani tulipambana na ilipofika Agosti 27 mwaka 2018 ilitoka hukumu kuwa mwanangu anatakiwa atumikie kifungo cha miaka 60 jela, hii hali iliniathiri mimi kama mzazi ambapo mimi ni baba mjane, hawa watoto mke wangu aliniachia wakiwa wadogo na nimeteseka nao sana mpaka huyu Tumain alipofika kidato cha nne,” anasema.

 

 

Anaendelea; “Kwa kweli niliumia sana maana ni mwanangu wa pili katika uzao wangu wa watoto sita,,nilipambana na hii kesi kwa muda mrefu mpaka ilipotoka hukumu ya kifungo cha miaka 60 gerezani.’’

 

 

“Nilikuwa sina hili wala lile kama mkulima niliomba msaada kwa ndugu jamaa na marafiki kwa ajili ya kukata rufaa ndipo nilipokata rufaa ikaenda Mahakama Kuu kanda ya Moshi ambapo baadaye alionekana anapasa kuendelea na kifungo ambapo alipunguziwa miaka 30. Kwa kuwa mwanangu hakutenda hili kosa niliendelea kumsaidia kukata rufaa nyingine zaidi , lakini kilichonikwamisha mpaka sasa nimekosa nguvu ya kuendelea kumsaidia ili haki ya mwanangu ipatikane,”alieleza mzee Mfinanga

 

 

“Kilio changu kwa Rais John Pombe Magufuli ambaye ni Rais wa wanyonge anionee huruma na anisaidie katika hili ili haki ya mwanangu ipatikane , huyu binti aliyefanya kosa amekuwa akija nyumbani kwangu na kuniomba msamaha kwa kile alichotenda dhidi ya mwanangu kwa vile amekiri mwenyewe naomba Rais wangu mtetezi wangu anisaidie,”alisema baba huyo.

 

 

Alipoulizwa sababu kwa nini hawakupima vinasaba (DNA) ili kubaini kama mtoto huyo ni wa mwanawe, baba huyo alisema;

 

 

“Hatukupima DNA kwa sababu ukweli aliujua binti ila ukweli ni kwamba hakimu aliyekuwa akisiliza kesi mara ya kwanza alihamishwa hivyo mpango wa kupima DNA ulifia hapo maana aliletwa hakimu mwingine ambaye ndiye aliyetoa hukumu.”

 

 

Alichokisema wakili

Elizabeth Minde ambaye ni mwanasheria Mkoa wa Kilimanjaro, alisema endapo kijana huyo atafanikiwa kuachiwa baada ya kukata rufaa, anaweza akamsamehe au akafanya maamuzi mengine kwa kumpotezea muda.

 

 

“Ni uamuzi wa mtu aliyeathirika kuchukua hatua, inategemea na uhusiano ndani ya jamii maana kuna leo na kesho maana mpaka asingiziwe kulikuwa na nini hapo?,”alihoji mama Minde.

Leave A Reply