The House of Favourite Newspapers

Bocco Amepona Majeraha Arudi Kuwavaa Orlando Pirates ya Nchini Afrika Kusini Leo

0
Kikosi cha simba.

HABARI njema kwa mashabiki wa Simba kuwa nahodha na mshambuliaji wao, John Bocco amepona majeraha yake ya enka na huenda akawa sehemu ya kikosi kitakachowavaa Orlando Pirates ya nchini Afrika Kusini.

 

Bocco ameikosa michezo miwili iliyopita ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USGN ya nchini Niger na RS Berkane ya Morocco ambayo yote ilichezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa Bocco anaendelea vizuri baada ya kupona na atakuwepo sehemu ya timu itakayocheza dhidi ya Simba.

 

Ally alisema kuwa Bocco alianza mazoezi pamoja na wenzake tangu timu ilipoingia kambini kujiandaa na mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Pirates.

 

Aliongeza kuwa mshambuliaji huyo akirejea, kocha mkuu wa timu hiyo, Mhispania Franco Pablo ameanza kuwaandaa mbadala wa kiungo Sadio Kanoute na beki Joash Onyango watakaoukosa mchezo huo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

 

“Wakati tukiwakosa Kanoute na Onyango, mshambuliaji wetu Bocco atakuwepo katika mchezo dhidi ya Pirates baada ya kupona majeraha yake ya enka.

 

“Bocco alikosa michezo baadhi ya hatua ya makundi ya Shirikisho kutokana na majeraha yake, hivyo katika mchezo dhidi ya Pirates atakuwepo uwanjani.

 

“Timu itawakosa wachezaji wawili pekee ambao ni Onyango na Kanoute ambao tayari wamepatikana watakaochukua nafasi zao na kocha anaendelea kuwandaa ili wazibe vizuri nafasi zao katika mchezo huo,” alisema Ally.

Stori; Wilbert Molandi

Leave A Reply