Bodi ya Filamu na Wadau Wake Kufanya Onesho la Kumuenzi Magufuli

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dkt. Kiagho Kilonzo akizungumza.

BODI ya Filamu nchini kwa kushirikiana na wasanii wa Bongo muvi kesho Jumatano Aprili 7 wanatarajia kufanya maonesho maalum kwa ajili ya kumuenzi aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Maonesho hayo yatafanyika Makumbusho ya Taifa yaliyopo Posta jijini Dar ambapo zitaoneshwa filamu fupifupi za Magufuli enzi za uhai wake mpaka mazishi yake pamoja na kumbukumbu zake nyingine.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Filamu nchini (TAFF) Eliah Mjata (kulia) naye akizungumza kwa niaba ya wasanii wa filamu. 

Akizungumza na wanahabari leo Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Dkt Kiagho Kilonzo amesema lengo la maonesho hayo ni kumuenzi Hayati Magufuli ambaye alikuwa mstali wa mbele kutetea kazi za wasanii.

“Kwakuwa Dkt Magufuli alikuwa mtetezi wetu hivyo sisi kama bodi ya filamu na wasanii wa filamu tumeona tuchukue nafasi hiyo kumuenzi kiongozi wetu huyo.”

Katika uhai wake Dkt Magufuli alikuwa begakwa bega na wasanii hivyo kutokana na pigo la kuondokewa naye tumeona japo tumuenzi kwa kuonesha filamu fupifupi zinazoelezea maisha yake.

Mkurugenzi wa Kituo cha Makumbusho ya Taifa kilichopo Posta jijini Dar, Achile Sibufule akiwakaribisha wadau kujitokeza kwenye maonesho hayo.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Filamu nchini (TAFF) Eliah Mjata amewataka wasanii na wadau wa filamu kuhudhuria kwenye maonesho hayo ambayo kiingilio ni bure.

Mjata amesema wasanii kwa ujumla wameona waungane na Bodi ya Filamu kwa ajili ya kumuenzi Dkt. Magufuli ambaye walikuwa naye bega kwa bega kwenye harakati za kuitetea kazi ya sanaa ya uigizaji.

Mkutano ukiendelea.

Achile Sibufule Mkurugenzi wa Kituo cha Makumbusho ya Taifa kilichopo Posta jijini Dar amewahamasisha wasanii na wadau wa filamu kujitokeza kwenye maonesho hayo na kuwaambia kuwa katika maonesho hayo wataweza kujifunza mambo mengi.

Sibufule amesema katika maonesho hayo watapokea kazi mbalimbali za filamu zinazohusu msiba na maisha ya Hayati Dkt. John Magufuli na kuzihifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Katika Maonesho hayo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo, Innocent Bashungwa.

Toa comment