The House of Favourite Newspapers

Bodi ya Mikopo Kumrudishia Fedha za Mwalimu Baada ya Kumkata Kimakosa

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema itarejesha kiasi cha shilingi 282,000 ilizomkata kimakosa Mwalimu Edwini Ndyamukama wa jijini Mwanza baada ya kugundua Mwalimu huyo hadaiwi na Bodi hiyo.
Taaarifa iliyotolwa na Bodi ya Mikopo inaeleza kuwa kanzidata ya Bodi ya Mikopo haimuoneshi Mwalimu Edwini Ndyamukama kama mdaiwa na baada ya uchunguzi imebainika kuwa anayedaiwa na Bodi hiyo ni Edwin F. Ndyamukama aliyesoma Chuo Kikuu Kishiriki cha Archbishop James (AJUCO) ambaye alikopeshwa na kupokea zaidi ya Shilingi milioni 2.29 hadi kufikia mwaka 2015.
“Ni kweli Mwalimu Ndyamukama mwenye namba ya mtihani wa Kidato cha nne S0304.1993 anadai kurejeshewa shilingi 282,000 alizokatwa kama marejesho ya mkopo wa elimu ya juu. Malipo haya na mengine yanakamilishwa na yatawekwa katika akaunti yake ya benki kabla ya Jumanne wiki ijayo,” inaeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa malipo hayo yanafanyika baada ya kukamilika kwa ukaguzi na uchunguzi uliothibitisha kuwa malalamikaji hakunufaika na fedha za mkopo na kwamba hao ni watu wawili tofauti.
“Ni vema kufahamu kuwa makato katika mshahara wa Mwalimu Edwini ambaye ni mlalamikaji yalisitishwa na alipewa taarifa, lakini kilichokuwa kinafanywa na Bodi ni kuondoa shaka ya yeye kuwa si mnufaika wa mkopo kwani kumekuwa na matukio ya watu kulalamika lakini baada ya uchunguzi inagundulika kuwa wengine ni wadaiwa,” inafafanua taarifa hiyo.
Katika malamiko yake, Mwalimu Edwini Ndyamukama alinukuliwa na Gazeti la Uhuru la Januari 3 mwaka huu akieleza kuwa Bodi ya Mikopo walimkata fedha katika mshahara wake wa mwezi May na June mwaka jana wakati yeye hakuwahi kukopeshwa na Bodi hiyo.
Mwalimu Edwini alieleza kuwa baada kuona amekatwa fedha aliandika barua ya malalamiko na Bodi walisitisha kukata mshahara wake lakini alikuwa bado hajalipwa fedha zilizokatwa kimakosa.

Comments are closed.