The House of Favourite Newspapers

Bombardier Yashindwa Kupaa kwa Hitilafu, Fastjet Yashindwa Kutua

JANA Februari 1, 2016, kulikuwa na matukio mawili yanayohusu kampuni za ndege zinazofanya safari zake nchini Tanzania.

Jijini Mwanza, ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Bombardier Q400 ilishindwa kuruka kutoka uwanjani hapo kutokana na kupata hitilafu.

Katika uwanja wa ndege wa Mwanza, abiria wa ndege ya Bombardier walishindwa kufanya safari yao ya kuelekea jijini Dar es salaam kutokana na ndege waliyokuwa waitumie kupata hitilafu. Ndege hiyo yenye namba 5H-TCB ilitakiwa kuruka kutoka Mwanza saa moja kamili jioni lakini ilishindwa.

“Mara ya kwanza ndege iliruka baadae ikatua, ikaruka tena kwa mara ya pili na baadae ikatua, ndipo mmoja wa wahudumu akatangaza tushuke ili waikague ndege hiyo kwani ilionesha kuna tatizo,” alisema abiria mmoja.

Alisema iliwalazimu kubaki uwanjani mpaka saa saba kasorobo usiku wakisubiri ndege nyengine ya kampuni hiyo iliyokuja kuwachukua na kufika Dar es salaam saa nane usiku.

Wakati hayo yakitokea jijini Mwanza, Mbeya nako ndege ya Shirika la Ndege la FastJet ilishindwa kutua katika uwanja wa ndege wa Songwe kufuatia kuwepo kwa ukungu mzito na mvua kubwa.

Ndege hiyo aina ya Airbus A319 ilitarajiwa kutua Uwanja wa Kimataifa wa Songwe saa mbili kamili asubuhi, lakini ililazimika kurudi Dar es Salaam.

Kaimu Meneja wa uwanja huo, Hamis Amiri alisema marubani wa ndege hiyo waliamua kurudi Dar es salaam na abiria kuepukwa hatari ambayo ingetokea endapo wangejaribu kutua.

“Kwanza kulikuwa na mvua kubwa halafu ukungu pamoja na mawingu vilitanda eneo la uwanja jambo ambalo lilisababisha marubani washindwe kuona vizuri njia ya ndege,” alisema.

 

Comments are closed.