The House of Favourite Newspapers

Mpoto Ataja Sababu za Wasanii Kumkimbia, Bendi Yake Kufa

Mrisho Mpoto

 

MAKALA: Hashim Aziz | AMANI

Mrisho Mpoto ndiyo jina lake kamili lakini wengi wanamfahamu kwa jina la Mjomba, ukimuita Sizonje pia anaitika! Staili yake ya kipekee ya kughani mashairi ya Kiswahili, yenye ujumbe mkubwa kwa jamii, ndiyo iliyomtambulisha na kumfikisha hapa alipo leo.

Mrisho Mpoto

Unaukumba wimbo wa Nikipata Nauli? Huo ndiyo uliomtambulisha Mpoto na kumtoa rasmi kwenye ulimwengu wa burudani! Akapata mafanikio makubwa kiasi cha kufungua bendi, Mjomba Band ambayo hata hivyo, baadaye ilikufa.

Amani limefanya naye mazungumzo ambapo mbali na mambo mengine, ameeleza sababu za bendi yake kufa, ametaja utajiri wake na kueleza mambo mengine mengi, fuatana nami katika mahojiano haya:

…Akiwa Global Tv

Amani: Mambo vipi mjomba?

Mpoto: Safi kabisa mjomba, vipi hali yako?

Amani: Fresh! Wananchi wengi hasa wasanii wenzako wanazungumzia kuwa maisha yamekuwa magumu sana na pesa zimepotea mitaani, vipi wewe unasemaje?

Mpoto: Wanaposema pesa zimepotea mitaani wana maana gani? Zimepotea kwenda wapi? Kwani kama mtu alikuwa anafanya kazi na analipwa mshahara uleule, au anafanya biashara ileile, leo anasemaje pesa zimepotea mitaani? Pesa hazijapotea sema watu wameanza kuwa na  nidhamu ya pesa.

Amani: Unauzungumziaje utawala wa Rais Magufuli?

Mpoto: Binafsi namkubali sana Magufuli kwa sababu yale niliyokuwa nayaimba kwenye nyimbo zangu ndiyo anayoyafanyia kazi. Nilishasema, kuanza upya siyo ujinga! Magufuli amekubali tuanze upya na anatuonesha dira, hata kama kuna watu watamchukia lakini baadaye wataelewa kwamba nia yake ni nzuri.

Amani: Kwa nini nyimbo zako nyingi unaimba na Banana Zorro na hata kwenye maonesho mengi mnaonekana pamoja?

Mpoto: Kwa ufupi ni kwa sababu ‘chemistry’ yangu na Banana inakubali, yaani akiimba chorus naisikia vizuri sana moyoni mwangu na ananipa mzuka wa kuimba, ni hivyo tu.

…Akitumbuzi

Amani: Ulipoamua kufunga ndoa, ulifanya sherehe nzima kitamaduni sana, nakumbuka badala ya keki watu walikula maboga na matikiti na badala ya shampeni watu walikunywa togwa. Kwa nini uliamua kuifanya iwe hivyo?

Mpoto: Siku zote mimi huwa najivunia sana utamaduni wa kwetu Watanzania na utamaduni wa mtu mweusi. Nilichofanya ilikuwa ni kudumisha tamaduni, kama watu wa mataifa mengine wanavyofanya kwa tamaduni zao.

Amani: Wakati unaanza kutoka kisanii, ulikuwa ukiimba nyimbo nyingi zenye mafumbo na ujumbe mzito kwa serikali, lakini sasa hivi ni kama umepoa na hutoi tena mashairi mazito, nini kimekusibu?

Mpoto: Unajua kunapokua na jambo baya, lazima ulikemee kwa nguvu zote na kunapokuwa na mambo mazuri yanayofanyika, ni lazima usifie. Huwezi kuwa mtu wa kukemea hata mazuri, hapana. Kipindi kile kulikuwa na mambo mengi mabaya yaliyokuwa yakiendelea na ndiyo maana nikawa naimba kukemea. Kwa upande wa Magufuli bado sijaona mabaya yake kwa hiyo nampa muda huku nikiendelea kumsoma.

Amani: Mpaka sasa muziki umekupa mafanikio gani?

Mpoto: Kwa kifupi, muziki umenipa kila kitu ambacho moyo wa binadamu unaweza kutamani. Muziki umenifanya niwe na nyumba, magari na vitega uchumi vingi. Muziki umenifanya nimiliki kijiji changu mwenyewe, kinaitwa Mpoto Village, kipo Mkuranga, kule tunalima na kufuga, karibu sana siku uje kujionea.

Amani: Una mpango wowote wa kugombea nafasi yoyote ya kisiasa?

Mpoto: Hapana.

Amani: Ulikuwa ukimiliki bendi iitwayo Mjomba Band, unaweza kueleza ni kwa nini wasanii walikukimbia na bendi ikafa?

Mpoto: Unajua wasanii wengi wana-penda unapo-kuwa na bendi, upige kwenye kumbi za starehe kama kwenye mabaa na mahoteli ili wengine walewe au wapate mademu au wanaume. Kwangu mimi nilikuwa na miiko kwamba siwezi kupiga muziki baa au kwenye pombe, kwa hiyo wasanii wengi wakawa wananikimbia na mpaka sasa bendi imesimama kufanya kazi. Ni hivyo tu, hakuna sababu nyingine.

Amani: Ahsante sana Mjomba kwa ushirikiano.

Mpoto: Ahsante, karibu sana kijijini kwangu.

Save

Comments are closed.