The House of Favourite Newspapers

Boomplay, CMG Zasaini Mkataba wa Ushirikiano

0

Jukwaa la Mtandaoni la Boomplay kwa kushirikiana na Clouds Media Group (CMG), wamesaini mkataba wa ushirikiano wa kimkakati ambao utawawezesha watumiaji wa jukwaa hilo kupata maudhui kutoka Clouds FM.

Kupitia ushirikiano huu, watumiaji wa Boomplay duniani kote watakuwa na uwezo wa kusikiliza vipindi pendwa kutoka Clouds FM ikiwemo XXL, Amplifaya, Traffic Jamz, Bongo Fleva na vingine vingi.

Meneja Mkuu wa Boomplay Tanzania, Natasha Stambuli ameyasema hayo leo Julai 22, 2021 kupitia taarifa kwa vyombo vya habari na kuongeza kuwa wamekusudia kuendelea kuwaunganisha wasikilizaji kupitia jukwaa hilo.

Ameongeza kuwa, Boomplay itaendelea kushirikiana na wadau wengine ili kuendelea kuweka vizuri mazingira yake ya kidijitali na vilevile kuunganisha mitiririko bora wa maudhui pendwa wakati wowote na popote duniani.

Maneno yake yaliungwa mkono na Afisa Mkuu wa Ubunifu na Mkakati wa Clouds Media Group, Reuben Ndege ambaye aliipongeza kampuni hiyo kwa kuongoza katika utoaji wa maudhui mbalimbali barani Afrika.

“Ushirikiano huu una maana kubwa kwetu, kwani unaturuhusu kuwa karibu na wasikilizaji wetu ambao wengi wao ni vijana na kupitia mamilioni ya watumiaji wa Boomplay tutaweza kuwafikia vijana wengi zaidi nchini Tanzania na duniani kote.

“Ushirikiano unatusaidia kubadilisha maudhui yetu kwa wasikilizaji kutoka kwenye kupanga kusikiliza kwenda kwenye usikilizaji wa muda wowote ambapo msikilizaji hatokosa sauti tulivu, inayopendwa, ya kipekee, inayobadilika na kusambazika ambao ndio utamaduni wa maudhui ya Clouds Media.

Hakuna mshirika mwingine tuliyemfikiria katika ushirikiano huu wa kimkakati zaidi ya Boomplay,” alisema Ndege. Huu ni ushirikiano wa kwanza wa aina yake na Clouds Media inakuwa kampuni ya kwanza ya vyombo vya habari kushirikiana na Boomplay kwa Afrika Mashariki.

Leave A Reply