The House of Favourite Newspapers

Boris Johnson Akatisha Likizo, Kujiunga Kinyang’anyiro cha Uwaziri Mkuu

0

WAZIRI Mkuu wa zamani wa Uingereza, Boris Johnson amerejea London wakati taarifa zikidai kwamba mpinzani wake Rishi Sunak tayari amefanikiwa kupata uungwaji mkono unaohitajika na chama ili kuwania nafasi ya juu kabisa nchini humo.

 

Ilimpasa Johnson kukatiza likizo yake ya kifahari katika Jamhuri ya Dominika, ili aungane na wenzake wawili katika kinyang’anyiro hicho cha kumrithi Liz Truss aliyejiuzulu, huku washirika wake wakivihakikishia vyombo vya habari kwamba ana nia hasa ya kugombea.

 

Johnson aliyefanikisha kuiondoa Uingereza kwenye Umoja wa Ulaya, aliachia wadhifa huo mapema mwezi Septemba, miezi miwili baada ya kutangaza kujiuzulu, kufuatia shinikizo la wabunge lililotokana na msururu wa kashfa dhidi yake.

 

Hata hivyo, dhamira yake ya kurejea madarakani siku chache tu baada ya kujiuzulu tayari imepingwa na wanasiasa wa upinzani na hata baadhi ya wabunge wa chama chake tawala kilichogawanyika ambao wanataka utulivu na umoja.

 

David Frost mmoja ya wabunge waliomuunga mkono huko nyuma, amesema “Sio sawa kukujiingiza tena kwenye vurugu na sintofahamu kama ya mwaka jana”. “Tunatakiwa kusonga mbele” aliwaomba wabunge wa Conservative na kuongeza kuwa wanatakiwa kumpata kiongozi mwenye uwezo wa kutekeleza programu za chama hicho, akimtaja waziri wa zamani wa fedha, Rishi Sunak.

 

Ijumaa usiku, washirika wa Sunak kwenye bunge walifichua kwamba tayari alikuwa amejikusanyia wabunge 100 wa Conservative wanaomuunga mkono, hii ikiwa ni idadi inayotakiwa na chama ili kugombea nafasi hiyo.

Hata hivyo, kwa pamoja Sunak na Johnson bado hawajatangaza hadharani kugombea, ingawa ripoti zinaashiria wazi nia ya kugombea.

Liz Truss alitangaza kujiuzulu siku 44 tangu alipoingia madarakani na kuwa waziri mkuu aliyehudumu kwa siku chache zaidi nchini Uingereza.

 

Chama cha Conservative kimelazimika kuingia upya kwenye mchakato wa kuchagua kiongozi baada ya waziri mkuu Truss kuzangaza ghafla kujiuzulu, baada ya siku 44 tu za kuliongoza taifa hilo. Mpango wake wa bajeti ndogo na kodi uliosababisha mzozo kwenye masoko ya fedha, ndio hasa uliomtia hatiani. Mzozo huo ulitabiriwa na Sunak mara tu baada ya Truss na serikali yake kutangaza bajeti hiyo.

Kulingana na vyombo vya habari vya Uingereza, BBC na gazeti la Sunday Times, usiku wa jana, wapinzani hao wawili walikutana kwa mazungumzo ya ana kwa ana jijini London. Ikumbukwe Rishi Sunak alikuwa waziri wa fedha wa serikali ya Johnson na kujiuzulu kwake kulichochea pakubwa Johnson naye kuamua kuanchia ngazi.

Wafuasi wa Johnson na Sunak, walitaka sana kufanyika kwa mazungumzo ili kuona kama wanaweza kufikia makubaliano ya kuwa na kauli moja, ingawa kulionekana na uwezekano finyu na hasa kutokana na hatua ya Sunak ya kujiuzulu licha ya kuwa mshirika wa karibu wa Johnson.

 

Wabunge wa Conservative 357 wanatarajiwa kushirika kwenye uchaguzi utakaofanyika siku ya Jumatatu kwa mgombea yoyote atakayefanikiwa kupata uungwaji mkono wa wabunge 100. Na iwapo wagombea wawili watafikisha idadi hiyo, kuna uwezekano wa wanachama wa chama hicho kupiga kura kwa njia ya mtandao baadae wiki ijayo.

EXCLUSIVE: TUNU SHENKOME AMALIZA UTATA MGUNDA vs NABI, AICHAMBUA DERBY ya KARIAKOO A – Z..

Leave A Reply