The House of Favourite Newspapers

Bosi wa Gesti Matatani Kifo cha Mfanyabiashara

SAKATA la kuuawa kwa mfanyabiashara Charles Nyanga Magesa (31) kisha maiti yake kutupwa katika kisima chenye maji machafu karibu na nyumba ya kulala wageni ya Mwita Wazanga katika eneo la stendi ya mabasi ya Sabasaba Kijiji cha Isaba, Wilaya ya Butiama, Mkoa wa Mara, limechukua sura mpya baada ya jeshi la polisi mkoani hapa kumtia matatani na kumshikilia mmiliki wa baa na gesti ambayo mauaji hayo yalitokea.

 

Bosi huyo, Meri Goteni Meri wa Kijiji cha Isaba tayari wamefunguliwa jalada la mauaji namba BUT/IR/2442018 kutokana na mauaji yaliyotokea usiku wa kuamkia Machi 21 mwaka huu baada ya marehemu kushambuliwa na kuuawa na watu wasiojulikana, katika baa ya mmiliki huyo eneo hilo.

Kwa mjibu wa taarifa za jeshi la polisi, bado wanaendelea kuwatafuta wote waliohusika na tukio hilo la kinyama popote walipo ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

 

Siri ya kuuawa kwa marehemu huyo imefichuka baada ya baadhi ya watu ambao hawakutaka kuandikwa majina yao kwenye gazeti hili kwa kuhofia usalama wao, kueleza wazi jinsi ugomvi ulivyotokea na kudaiwa kuwa chanzo cha marehemu huyo kushambuliwa na hadi kuuawa na kisha mwili wake kutupwa kwenye kisima hicho cha maji machafu ni kugombea mwanamke kati ya wauaji na marehemu huyo.

Mwanamke aliyegombewa ambaye anatafutwa na polisi alifahamika kwa jina moja la Bonge na ametajwa kuwa ni mhudumu wa baa ya mmiliki huyo ambapo marehemu alishambuliwa kwa vipigo, hadi kufariki dunia bila bila mwenye baa hiyo kupiga simu polisi au kwa viongozi wa serikali, wala kupiga yowe ili majirani wasaidie.

 

Habari zinasema ugomvi uliosababisha kifo hicho ulianza majira ya saa 5.00 usiku wa Machi 20, mwaka huu marehemu huyo aliposhambuliwa na watu watatu na kisha kuachanishwa wakati walipokuwa wakinywa vinywaji wote katika baa hiyo lakini ugomvi huo uliendelea tena saa 7.00 usiku na watu hao wakatoweka na marehemu ambaye baadaye mwili wake ulikutwa ukiwa kisima cha maji machafu.

Marehemu huyo baada ya kuuawa, alivuliwa nguo zake na viatu vyake na kutupwa katika kisima akiwa amefungwa kamba miguuni.

 

Taarifa za uchunguzi wa kidaktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu huyo baada ya kumtoa kwenye shimo hilo ulibaini kuwa, alikuwa na majeraha ya nje ya vipigo alivyoshambuliwa na wauaji hao kwa vitu vizito kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wake yaliyosababisha kupoteza maisha yake.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, SACP, Jafar Mohamed amethibitisha kukamatwa kwa Meri na akasema upelelezi bado unaendelea

Stori: WAANDISHI WETU, Dar

Comments are closed.