The House of Favourite Newspapers

Bosi Wa Waamuzi Avunja Ukimya Utata wa Mikwaju iliyopigwa na wachezaji wa Yanga

0
Salum Umande Chama

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Salum Umande Chama, amevunja ukimya kutokana na utata uliojitokeza muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ngao ya Jamii, kati ya Yanga dhidi ya Simba.

Utata ulioibuka ni namna kipa wa Simba, Ally Salim alivyokuwa akiokoa mikwaju iliyopigwa na wachezaji wa Yanga ambapo alifanikiwa kuzuia penalti tatu za Khalid Aucho, Pacome Zouzoua na Yao Attohoula.

Katika mchezo huo wa fainali ya Ngao ya Jamii uliochezwa juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Simba iliibuka na ushindi wa penalti 3-1 dhidi ya Yanga, baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa 0-0.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, wadau mbalimbali wa soka wamekuwa wakihoji wakidai kwamba, waamuzi waliruhusu Ally Salim kutoka kwenye mstari kabla ya pigo la penalti.

Kipa wa Simba, Ally Salim

Mbali na hilo, pia mwamuzi wa kati, Jonesia Rukyaa, alilalamikiwa kwa namna ya uamuzi wake ambapo wapo waliosema aliegemea upande mmoja, huku maamuzi yake mengi yakiwa si sahihi.

Akizungumza na Spoti Xtra, bosi huyo wa zamani wa waamuzi ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera, amesema tangu mwanzo hadi mwisho wa mchezo huo, hakukuwa na chembe yoyote ya upendeleo iliyofanywa na waamuzi, huku akibainisha kwamba, kulikuwa na dosari ndogo ambazo hazikuathiri chochote.

“Kwa ujumla dosari zilikuwa ndogo ambazo wala hazikuleta athari zozote za mchezo.”

Kuhusu madai ya Ally Salim kutoka kwenye mstari kabla ya pigo la penalti, Umande alisema: “Siyo rahisi hilo kulizungumzia, ndiyo maana wenzetu Ulaya wana VAR ambayo huonesha vitu kama hivyo.

“Pigo la penalti wakati linapigwa, si rahisi kuona makosa madogo kama hayo, sasa hao wanaozungumzia hilo jambo utagundua wamefanya hivyo baada ya mchezo kuisha, walikaa na kutafakari, lakini mchezo unapokuwa unaendelea sio rahisi sana kutambua kitu kama hicho hasa kwa mwamuzi. Mimi ninaona mchezo umechezeshwa vizuri, mambo yote yameenda ‘fair’.”

MWANDISHI WETU, GAZETI LA CHAMPONI, SPOTI XTRA

BABA LEVO AMVAA LISSU na LEMA SAKATA la BANDARI – “HAWANA MSIMAMO, MARA KATIBA MARA DP WORLD”…

Leave A Reply