The House of Favourite Newspapers

Hussein Bashe Afunguka LIVE Kuhusu Mauaji Yanayoendelea – Video

AKIZUNGUMZA na waandishi wa habari leo, Machi 8, 2018, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amesema.

 

“Wanaosema Bunge halina meno, halina nguvu tena si kweli. Bunge ndiyo chombo pekee kinachoweza kuisimamia serikali kisheria na mambo yote ya kibunge yanajadiliwa bungeni kwa utaratibu uliowekwa na sheria za nchi.

 

“Viongozi kulalamika hakuondoi matatizo ya watu, tuyapeleke bungeni tukayajadili bungeni kwa mujibu wa sheria. Hoja yangu imefuata taratibu zote muhimu za kibunge na kichama, bungeni nimemuandikia barua Katibu wa Bunge na kwa upande wa chama tumeshauriana na kumuandikia Barua Katibu wa Wabunge wa CCM bungeni ili kushirikisha Chama katika kujenga hoja.

 

“CCM ni chama cha wananchi na ndiyo chama chenye dola, kila linapotokea jambo wananchi wote hutegea sikio kusikia chama kinachowaongoza kitasema nini na kitatoa muelekeo gani? Ni wakati sasa tukaondoa hofu za wananchi na kuwaunganisha pamoja.

 

“Sishangai watu wengine ndani ya chama kama watajitokeza kupinga hoja hii, ni jambo la kawaida na ndiyo demokrasia. CCM kina demokrasia kubwa ya kupingana na kukosoana wenyewe kwa wenyewe kwa maslahi mapana ya chama.

 

“Tangu enzi ya Mzee Nyerere, Mwinyi, Mkapa na Kikwete hata sasa Rais Magufuli, bado CCM imekuwa imara na inaheshimu utaratibu wa kupingana kwa hoja na kukosoana, huu ndiyo ukomavu wa CCM na ni tofauti na vyama vingine.

 

“Mbunge anaposema kuwa bunge halina meno wakati yeye ni sehemu ya bunge hilo lazima umshangae! Kama unaona bunge limekosa meno haliwezi kufanya kazi za kibunge toka nje, acha wanaojua umuhimu wa kutumia bunge kuweza kuwasilisha mawazo na hoja zao bungeni.

 

“Wanaosema bunge halina nguvu ndiyo hawa ambao mara nyingi wakiwa bungeni huomba serikali kutekeleza miradi kwenye maeneo yao na serikali inatekeleza. Sasa kama unaongelea bungeni na serikali zinafanya, unasemaje bunge halina meno? Tusidharau kuti tulilolikalia wakati ndiyo linatupa nafasi ya kuwasilisha hoja na kuisimamia serikali.

 

“Hoja yangu inatoa nafasi ya kuanza upya n mwanya wa vyama vya siasa vyote kutatua matatizo yaliyopo na kudumisha mshikamano na umoja wa kitaifa kupitia mjadala wa kibunge na kwa kuwa CCM ndiyo chama tawala basi tunayo nafasi kama chama kuijenga Tanzania tuitakayo.

 

“Siku za hivi karibuni viongozi wa CCM waliouawa, kuteswa na wengine kufanywa walemavu ni wengi sana kuliko wale wa upinzani lakini hujawahi kusikia vyama vya upinzani nchini vikiongelea haya, Je, hawa wa CCM ni haki yao kuuawa au je wao vifo vyao havina uchungu?

 

“Ukiwasikia upinzani wanavyoyaongelea mambo ya watu kuteswa au kuuawa wanayaongelea kwa upande wao tu na kusahau kuwa hata viongozi wa CCM wanaumizwa, kuteswa na wengine kuuawa. Kwa hiyo mambo haya hayana chama ni mambo ya umoja wa kitaifa kabla ya kuwepo vyama vya siasa Tanzania ilikuwepo na itakuwepo baada yetu,” alisema Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe.

 

VIDEO: MSIKIE BASHE AKIFUNGUKA

Comments are closed.