The House of Favourite Newspapers

Breaking News: Boris Johnson Waziri Mkuu Mpya wa Uingereza -Video

ALIYEKUWA Meya wa zamani wa jiji la London, Boris Johnson (55) amechukua rasmi nafasi ya kuwa Waziri Mkuu wa nchini Uingereza baada ya Theresa May kujiuzulu leo Jumatano, Julai 24, 2019 baada ya Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza kumuomba kuunda serikali.

Waziri Mkuu huyo mpya ana miezi mitatu tu ya kutengeneza ambayo Theresa May aliposhindwa na kufanikisha ahadi zake za kuiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31.

Boris Johnson tayari ameshamteua Dominic Cummings kama mshauri mkuu wake.

Alipokuwa anafungasha virago na kuondoka katika ofisi yake ya Downing Street, Bi Theresa May alisema anafurahi kuwa mrithi wake Boris Jonhson ana nia ya kutimiza kile raia wa Uingereza walichokitaka, baada ya kupiga kura ya maoni mwaka 2016 kuondoka katika Umoja wa Ulaya.

 

Theresa May alisema bado ataendelea na majukumu yake mengine serikalini kama mbunge wa kawaida.

Boris Johnson akiongea nje ya Dawningstreet, amesema Uingereza itaondoka kwenye Umoja wa Ulaya tarehe 31 mwezi Oktoba hakuna shaka kuhusu hilo.

Wale wote wenye mashaka, na wanaosema kuwa jambo hili halitafanikiwa wamekosea, alisema waziri mkuu mpya.

Pia ameahidi kushughulikia suala la maslahi ya wazee wa nchi hiyo.

 

Wakati huo huo, Waziri wa Fedha wa Uingereza, Philip Hammond anayeupinga mpango wa Brexit amejiuzulu muda mchache kabla ya Boris Johnson kuwa waziri Mkuu wa Uingereza.

 

Hammond aliandika katika Ukurasa wake wa Twitter kuwa alimkabidhi rasmi barua ya kujiuzulu kwake Waziri Mkuu wa zamani Theresa May na kumshukuru kufanya nae kazi kwa miaka mitatu.

Wengine waliokataa kufanya kazi na Johnson na kujiuzulu ni Waziri wa Sheria, David Gauke na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa Rory Stewart.

 

Wote walisema wamejiuzulu kutokana na kutokubaliana na mipango ya Waziri Mkuu mpya juu ya suala la Brexit.

Urusi kwa upande wake kupitia wizara ya kigeni imesema hakuna mabadiliko yoyote katika uhusiano wake na Uingereza kufuatia Johnson kuwa Waziri Mkuu.

Urusi imesema Waziri Mkuu huyo mpya anatokea upande wa wale waliyoyaharibu mahusiano ya nchi hizo mbili.

Comments are closed.