BREAKING NEWS: SPIKA ASEMA ‘TUMPUUZE, TUMSAMEHE MASELE’

KAMATI ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyomtia hatiani kwa makosa manne Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM) ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Stephen Masele,  na kupendekeza asihudhurie mikutano mitatu ya Bunge kuanzia Mei 23, 2019, imelifikisha suala hilo bungeni ambapo, baada ya Spika Job Ndugai, kumwombea msamaha, bunge lilikubali na kumsamehe.

 

 

Awali, akiwasilisha taarifa yake, mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka,  amesema baada ya kumhoji Masele, walimkuta na makosa manne likiwemo la kuchonganisha mihimili ya dola, kusafiri nje ya nchi bila ya kibali cha spika na kuandika jumbe mfupi mbalimbali kwa viongozi wakuu wenye uchonganishi na kudharaua wito wa spika.

 

Hata hivyo, Masele alipewa nafasi ya kuomba radhi bungeni huku  ‘akizipangua’ hoja zilizomtia hatiani ikiwa ni pamoja na kumtuhumu spika kuwa amewasiliana na Rais wa PAP, Roger Nkodo Dang,  ili amng’oe katika nafasi yake ya Makamu wa Rais wa PAP ambaye anatuhumiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia.

 

Kwa upande wake, Ndugai amesema Masele ni  mwongo, mfitinishi, mchonganishi na kiongozi ambaye mara nyingi amekuwa akitumia muda wake kugonganisha mihimili na viongozi kwa jumla.

Ndugai alihitimisha jambo hilo kwa kutaka Bunge kumpuuza na kumsamehe Masele,  na kutaka Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhitimisha suala hilo kwa kutoijadili hoja hiyo na, hivyo, bunge likaridhia kumsamehe.

 

 

Masele alihojiwa na kamati hiyo Jumatatu Mei 20, 2019 akituhumiwa na Ndugai kwamba amekuwa na utovu wa nidhamu na kutoa maneno ya kugonganisha mihimili. Ndugai alilieleza Bunge Mei 16, 2019, kwamba kutokana na utovu huo wa nidhamu amesimamisha uwakilishi wa Masele katika PAP ambako mkutano wa Bunge hilo ulikuwa ukiendelea nchini Afrika Kusini na kuagiza mbunge huyo kurejea nchini ili kuhojiwa na kamati hiyo na baadaye na kamati ya maadili ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Toa comment