The House of Favourite Newspapers

Breaking News: Larry King Afariki Dunia

0

MTANGAZAJI na mwandishi wa habari mkongwe wa kituo cha runinga cha CNN cha nchini Marekani, Lawrence Harvey (87), almaarufu Larry King amefariki dunia leo Januari 23, 2021 katika Hospitali ya Cedars- Sinai, Los Angeles, nchini humo akiwa na umri wa miaka 87 kwa kile kilichoelezwa kuwa ni maradhi ya Covid-19.

 

Katika taarifa iliyotolewa na Ora Media, Kampuni ya Habari aliyokuwa anaimiliki, inaeleza kuwa nguli huyo wa habari, alilazwa hospitali tangu mwanzoni mwa mwezi Januari baada ya kupata maambukizi ya Covid 19.

 Kwa kipindi kirefu mwanahabari huyo alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya mapafu na saratani ya tezi dume huku mwaka 2019, akinusurika kupoteza maisha baada ya kupatwa na shambulio la moyo lililosababisha apoteze fahamu kwa wiki kadhaa.

 

Enzi za uhai wake, Larry King alijipatia umaarufu mkubwa kwa kuwahoji marais wengi wa Marekani tangu enzi za Rais Richard Nixon pamoja na wake zao, lakini pia akiwahoji viongozi wengine wakubwa duniani kutoka katika mataifa mbalimbali, akiwemo Dalai Lama na wengineo.

Umaarufu wa Larry King haukuishia kwa kuwahoji wanasiasa na viongozi wakubwa duniani pekee, bali pia alifanya mahojiano na wasanii maarufu, wanamichezo na watu wengine maarufu duniani.

Larry King aliianza kazi ya utangazaji mwaka 1957 na ameendelea kuwa mwandishi na mtangazaji wa redio na runinga kwa kipindi chote cha maisha yake.

Taarifa kuhusu mipango ya mazishi ya nguli huyo, zitatolewa hapo baadaye.

Leave A Reply