The House of Favourite Newspapers

BREAKING NEWS: NASSARI AFUNGUKA “NAKWENDA MAHAKAMANI”

Aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Samwel Nassari akiongea na wanahabari.

 

Aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Samwel Nassari amefunguka juu ya kuvuliwa ubunge kwa kudaiwa kutoshiriki vikao vya mikutano mitatu mfululilizo.

 

Akizungumza leo na vyombo vya habari Makao Makuu ya Chadema jijini Dar, Nassari amesema; “si sahihi hata kidogo na muda utakapofika huko mbele tutaweka nyaraka hadharani.”

 

Alisema kwa mfano kwa Bunge la Mwezi Septemba na vikao vyake alilipwa posho na stahiki zake zote kuonesha kwamba alikuwa akishiriki shughuli za kibunge.

 

“Ni kweli kwa Bunge la Mwezi Novemba, mwisho wa mwaka na Januari, mwanzo wa mwaka, sikuwepo bungeni kwa sababu ambazo kila mmoja wetu angeelewa na kuona uzito wake.

 

Kwa muda sasa, mimi na mke wangu tumekuwa na complications (matatizo) za kiafya na sina haja ya kuongelea kiundani kwani hayo ni mambo ambayo ni siri kati ya daktari na mgonjwa, lakini mimi na yeye tulitamani kupata mtoto kama wanandoa wengine na ili kutimiza azma hiyo ilitubidi kupata matibabu na uangalizi wa kiafya nje ya nchi na kama mume nililazimika kusimama na mke wangu hususan katika siku za mwisho za ujauzito wake mpaka alipofanikiwa kujifungua salama na tukafanikiwa kupata mtoto wa kike wa kwanza tarehe 27, mwezi wa kwanza 2019, siku moja kabla ya kuanza kwa kikao cha bunge Dodoma.

 

“Katika hali kama hiyo nilikuwa na machaguo mawili tu, moja, kumwacha mke wangu mahututi ili nihudhurie vikao vya bunge na kusaini posho au chaguo la pili lilikuwa kusimamia kiapo changu ambacho niliapa kanisani kwamba nitakuwa naye kwa shida na raha.

 

“Kwa hiyo nilichagua kusimama na familia na mke. Ninaamini yeyote ambaye angekuwa njiapanda kama niliyokuwa nayo mimi, angechagua kama ambavyo nilichagua mimi.

 

“Ningekuwa mpuuzi kama ningekimbilia bungeni na kusaini posho, ni kweli napenda pesa kama binadamu mwingine, lakini ningeonekana mpuuzi kumwacha mke wangu wa ndoa ambaye tumekula kiapo na huu ni mwaka wa tano tukiwa pamoja. lakini cha kusikitisha bunge halikunipa nafasi ya kunisikiliza. Hivi ningekuwa nimetekwa au nimepotea si walipaswa kutafuta huyu mtu ana shida gani?

 

“Kwa hiyo, pamoja na kuwa na huzuni kuvuliwa ubunge, lakini ninayo furaha kwamba nina mtoto.

Hata hivyo, nilifanya jitihada kubwa za kuitafuta ofisi ya Spika, Job Ndugai na nilizungumza na msaidizi binafsi wa spika, bwana Said Yakub nikiwa nje ya nchi kwa kutumia SMS ambazo zipo, akanipa e-mail ya bunge na akanihakikishia spika ataisoma.

 

“Ninaamini kwamba mheshimiwa spika ana nafasi ya kurejea maamuzi yake kama mzazi na mlezi wa wabunge wote.

“Ninachukua fursa hii kuwapa pole sana wananchi wa Jimbo la Meru kwani bado wanajua nilikuwa na dhamira nzuri ya kuwatumikia sasa na baadaye, lakini ieleweke kwamba ukiwa mbunge haiondoi ubinadamu.

 

“Kila nikiwaza maamuzi haya ya spika kunivua ubunge napata huzuni kubwa, lakini wananchi maelfu wa Meru wajue nipo tayari kupigania maslahi yao na kwa kuanza tunakwenda kwenye vyombo vya sheria mahakani kupata haki ya wananchi wa Meru kwani bado ninawapenda na nitaendelea kuwatumikia,” alimalizia Nassari.

 

STORI NA SIFAEL PAUL | GPL  

 

Comments are closed.