The House of Favourite Newspapers

Breaking: Prof Lipumba Ashinda Kesi, Sasa Ni Mwenyekiti Halali wa CUF

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo, Machi 18, 2019,  imetoa hukumu inayotambua Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa Chama cha Wananchi (CUF) baada ya kushinda kesi iliyotokana na mvutano wa uongozi dhidi ya  upande uliokuwa unamuunga mkono aliyekuwa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hammad.

 

Hukumu hiyo inatokana na kesi Namba 23/2016 iliyokuwa mbele ya Jaji Benhajj Masoud AMBAYE amesema kuwa msajili wa vyama vya siasa ana mamlaka ya kutoa msimamo na ushauri alioutoa kuhusu uhalali wa Profesa Lipumba.

Amesema mamlaka ya msajili hayaishii tu katika kusajili vyama na kupokea mabadiliko ya viongozi na kwamba vinginevyo asingekuwa na mamlaka ya kuvifuta vyama.

 

Kiini cha mgogoro huo ni  mgawanyiko wa wanachama ambapo upande mmoja ulikuwa kwa upande Lipumba na mwingine kwa Maalim Seif ambaye alikuwa Katibu Mkuu.

 

Taarifa zinaonyesha mpaka kufikia leo, hukumu hiyo ilikuwa imeahirishwa mara nnne na mara ya kwanza, ilitakiwa kusomwa Oktoba 10, 2018, ikaahirishwa hadi Novemba 30, 2018, ikaahirishwa tena hadi Januari 15, 2019,  ikaahirishwa tena hadi  Februari 22, 2019 na iliahirishwa hadi leo Machi 18, 2019.

 

Profesa Lipumba alijiuzulu nafasi ya uenyekiti Agosti 6, 2015 wakati chama kinaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais na kutimkia nje ya nchi ambapo baada ya ya uchaguzi alirejea nchini na kurudi kwenye chama chake akidai kuitwaa tena nafasi yake ya awali ya uenyekiti.

 

Wiki iliyopita Profesa Lipumba alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa kupata kura 516, akiwashinda wapinzani wake, Zubeir Hamis aliyepata kura 36 na Diana aliyepata kura 16. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar, ilichukuliwa na Abbas Juma Mhunzi aliyepata kura 349, wakati Makamu Mwenyekiti Bara, aliyeshinda ni Maftah Nachuma kwa kura 231.

 

Juzi Baraza Kuu la Uongozi, lilimchagua Khalifa Suleiman Khalifa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kwa kura 37, na  mpinzani wake, Masoud Said Suleiman, akipata kura 11.

Comments are closed.