The House of Favourite Newspapers

Buchosa Wakubali Kuhamia Mkoa wa Geita

0

 

Buchosa. Madiwani wa halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema Mkoa wa Mwanza wameridhia kuhamia Mkoa wa Geita kwa sharti la halmashauri hiyo kupandishwa hadhi kuwa wilaya sambamba na kuongezwa tarafa, kata na vijiji.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya kuitishwa baraza maalumu la madiwani la halmashauri hiyo kwa lengo la kujadili agenda ya maombi ya kuanzishwa mkoa mpya wa Chato kwa kumegwa jimbo la Buchosa.

 

Mkurugenzi wa halmashauri ya Buchosa, Paul Malala ametaja faida za kuhamia Mkoa wa Geita kuwa ni pamoja na kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi sambamba na kupunguza umbali kutoka Buchosa hadi Mwanza (kilomita 110) huku kwenda Geita ni kilomita 58, itasaidia huduma za wananchi kupatikana kwa urahisi.

 

Malala ametaja faida nyingine halmashauri hiyo itapata fursa ya kuwa wilaya itaongeza huduma za kijamii kama mahakama, kituo cha polisi, Magereza ,ofisi ya mkuu wa wilaya Ili kurahisisha upatikanaji wa huduma nyingi za kijamii ambazo hazikuwepo hapo awali katika eneo hilo.

 

Katibu wa CCM Wilaya ya Sengerema, Barnabas Nyerembe amepongeza hatua ya baraza maalumu la madiwani kukubali kwa kauli moja halmashauri ya Buchosa kuhamia Mkoa wa Geita kwa sharti la kuwa wilaya yenye mamlaka kamili.

 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Buchosa, Idama Kibanzi amesema maoni ya kamati ya fedha utawala na mipango baada ya kujadili faida na athari za halmashauri kuhamia Geita Ili kuwezesha kuanzishwa mkoa mpya wa Chato iliridhia kumegwa kwa jimbo la Buchosa kuwa sehemu ya Mkoa wa Geita endapo halmashauri hiyo itapewa hadhi ya kuwa wilaya yenye mamlaka kamili.

 

Diwani wa kata ya Bupandwa, Masumbuko Bupamba na Dotto Bulunda (Kafunzo) waliunga mkono hoja kwa kuridhia kuhamia Mkoa wa Geita.

 

Wameseme hata awali Buchosa na Sengerema zilimegwa kutoa Geita hivyo hawaoni tatizo lolote juu ya halmashauri hiyo kuhamia Mkoa wa Geita ila inatakiwa kupewa mamlaka kamili kama Wilaya.

 

Leave A Reply