The House of Favourite Newspapers

Bunge 2016 ndivyo sivyo

0

tuliaNaibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

Na Mwandishi wetu, RISASI MCHANGANYIKO

DAR ES SALAAM: Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaloendelea mjini Dodoma, likijadili bajeti ya mwaka huu wa fedha, linaelezwa kuwa ni la ndivyo sivyo, Risasi linakuja na taarifa kamili.

bungeniKumekuwa na mgongano wa mawazo miongoni mwa wananchi juu ya kitendo cha wabunge wa upinzani ambao wamekuwa wakitoka nje ya bunge, wakati mhimili huo unapokutana kufanya kazi zake chini ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

Wapinzani hao, chini ya umoja wao wa Ukawa, wamekuwa wakidai kuwa Dk. Tulia anawaburuza kwa kutosikiliza hoja zao na kwamba anatumia ubabe kupitisha au kuondoa baadhi ya hoja zinazowasilishwa na wabunge wa kambi hiyo.

1Kufuatia hali hiyo, baadhi ya wananchi, wakizungumza baada ya juzi Jumatatu wabunge hao kutoka wakiwa wamejiziba midomo kwa makaratasi, walisema kinachofanywa na wawakilishi hao wa wananchi ni sawa, kwani hamna namna nyingine nzuri ya kuonesha kutokubaliana kwao na kitendo cha uongozi wa Bunge kukiendesha chombo hicho kibabe.

“Kama hawasikilizwi, hawana jinsi ya kufanya, kutoka nje ya bunge ni namna inayokubalika kikanuni endapo wabunge hawakubaliani na jambo, lakini kwa hiki kinachotokea, nadhani uongozi wa bunge kwa ujumla wake, unapaswa kuwatazama zaidi wananchi kuliko wabunge.

“Kama wapinzani wana matatizo na Dk. Tulia, wangetumia busara, wenyeviti wangeongoza vikao vya bunge wakati suluhisho likitafutwa, lakini kuendelea kumtumia naibu spika huyo ni kama wanawafukuza makusudi wapinzani,” alisema Kohli Samson, mkazi wa Mbagala.

Auness Jacob, mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi wa Manzese jijini Dar es Salaam, licha ya kuwalaumu wapinzani kwa kutoka nje kila mara, lakini alipongeza msimamo wa uongozi wa bunge wa kuendelea kumtumia Naibu Spika Dk. Tulia kuongoza vikao vyake.

Alisema kuwatumia wenyeviti wa Bunge ni sawa na kunywea kwa wapinzani, kwani madai yao hayana msingi zaidi ya kutafuta umaarufu.

“Hawa hawana hoja, walianza na Bunge Live, wameshindwa sasa wanaanza sarakasi zingine, sasa kama Dk. Tulia atakaa pembeni, kesho wakisema hawamtaki Ndugai, naye akae pembeni? Huu ni wakati wa kazi,” alisema na kuongeza kuwa hata hivyo, kutoka kwa wapinzani kumepunguza msisimko wa majadiliano ya bajeti.

Kwenye mitandao ya kijamii, watu wengi walionesha kupagawa na staili mpya iliyofanywa na wabunge wa upinzani, ambao walifunga midomo yao kwa karatasi, zilizokuwa zimeandikwa ujumbe mbalimbali.

Wabunge wa upinzani walianza kutoka nje ya Bunge wakati wa uwasilishaji wa bajeti za wizara, wakipinga hatua ya naibu spika kukataa hoja zao mbalimbali, ikiwa ni pamoja na miongozo na taarifa, kwa walichosema anawaburuza.

Leave A Reply