Bupandwa FC Bingwa Mashindano ya Shigongo Cup Buchosa, Wakabidhiwa Kombe na Kitita – Video
HATIMAYE mashindano maalum ya Shigongo Cup yaliyokuwa yanashirikisha timu 22 kutoka Kata 21 za Jimbo la Buchosa yametamatika kwa mchezo mkali wa fainali ulioishuhudia Bupandwa FC wakiibuka mabingwa wa mashindano hayo.
Bupandwa ilifanikiwa kutinga fainali baada ya kuichapa timu ya Kata ya Bangwe bao 3-2 katika mchezo wa nusu fainali, huku Nyanzenda wao walifika fainali baada ya kuichapa Kalebezo bao 2-0 katika mchezo wa nusu fainali ya mashindano hayo.
Mchezo wa fainali ulianza majira ya saa tisa kamili jioni ulikuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili kutokana na timu hizo kuwa na upanzani wa miaka mingi kila wanapokutana, katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya Jimbo hilo.
Historia inaonesha timu hizo zimekutana mara tatu kabla ya fainali hii na mara zote hizo Nyanzenda fc walishinda. Katika fainali ya mwaka huu mashindano ya shigongo cup Bupandwa wakavunja uteja na kuichapa Nyanzenda bao 2-0.
Bingwa wa mashindano hayo ameondoka na kitita cha shilingi milioni 1.5 na kikombe, mshindi wa pili amepata laki nane, mshindi wa tatu amejinyakulia kitita cha laki tano huku mfungaji bora na mchezaji bora wakichukua laki moja kila mmoja.
Akizungumza baada ya kutoa zawadi hizo mgeni rasmi ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga akimuwakilisha mkuu wa mkoa wa mwanza, Amos Makala alisema: “Niwaombe tuendelee kudumisha amani na utulivu katika wilaya yetu, tumshukuru mbunge wetu, Eric Shigongo kwa kudhamini michezo hii na kwa kusaidia kutunza amani, sio hivyo tu bali vijana wetu wanajiajiri kupitia vipaji walivyopewa na Mungu na tuendelee kufanya mashindano haya kama sehemu ya kumuunga
mkono Rais Samia.
Kwa upande wake Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo alisema: “Matamanio yangu ni kuona vijana kutoka Buchosa wanacheza timu mbalimbali hapa nchini na kubwa zaidi natamani sana kuona Buchosa tuna timu ligi daraja la kwanza na ligi kuu.
“Nataka mpaka nikitoka madarakani Buchosa kuwe na uwanja wa michezo wa kisasa, ili timu kubwa ziwe zinakuja kucheza huku kwetu Buchosa.”
ReplyForward |