The House of Favourite Newspapers

CAG ni Nani, Ana Nguvu Gani?…Soma Hapa Kupata Majibu

0

MJADALA unaotikisha hivi sasa ni kuhusu kutolewa kwa ripoti ya CAG inayoelezwa kuwa imeainisha namba ambavyo fedha za umma “zimepigwa.”

Pamoja na mjadala kuwa wa moto kuna baadhi ya watu hawaelewi huyu CAG ni nani na ana kazi gani katika nchi. Ufafanuzi ni huu:

 

Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ni ofisi ambayo imeundwa kikatiba kupitia Ibara ya 143 na 144 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa mara kwa mara.
Ibara hiyo kwa ufupi inaeleza ifuatavyo;

 

143.- (1) Kutakuwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano. (2) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atakuwa na jukumu juu ya mambo yafuatayo:

 

(a) kuhakikisha kwamba fedha zozote zinazokusudiwa kutolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali matumizi yake yameidhinishwa na kwamba zitatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 136 ya Katiba hii, na iwapo atatosheka kwamba masharti hayo yatatekelezwa ipasavyo, basi ataidhinisha fedha hizo zitolewe;

 

(b) kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo matumizi yake yameidhinishwa yatokane na fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au fedha ambazo matumizi yake yameidhinishwa na sheria iliyotungwa na Bunge, na ambazo zimetumika, zimetumiwa kwa ajili ya shughuli zilizo husika na matumizi ya fedha hizo na kwamba matumizi hayo yamefanywa kwa kufuata idhini iliyotolewa kuhusu matumizi hayo; na

 

(c) angalau mara moja kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, hesabu zinazosimamiwa na watumishi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na hesabu za Mahakama zote za Jamhuri ya Muungano na hesabu zinazosimamiwa na Katibu wa Bunge.

 

(3) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu na kila mtumishi wa Serikali aliyeruhusiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atakuwa na haki ya kuchunguza vitabu, kumbukumbu, hati nyinginezo zote zinazohusika na hesabu za aina yoyote iliyotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara hii.

 

(4) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atawasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hii.

 

Baada ya kupokea taarifa hiyo Rais atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa hiyo na itabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho.

Unaweza kujielimisha zaidi kwenye Ibara tajwa kwenye katiba.

Leave A Reply