The House of Favourite Newspapers

Cannavaro hajaonana na Mo Dewji

MENEJA na nahodha wa zamani wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amerejea kwenye kikosi chake hicho na kuendelea na majukumu kama kawaida licha ya kuwa kulitokea hali ya sintofahamu kati yake na kiongozi wa benchi la ufundi la timu hiyo, Kocha Mwinyi Zahera.

 

Cannavaro aliwasili asubuhi katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika jana Jumatano kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini na kuendelea na majukumu yake. Kwa mujibu wa mtoa taarifa kutoka kwa rafiki wa karibu wa Cannavaro, ni kuwa alifika mazoezini hapo na kuendelea na majukumu yake, licha ya Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera kudai kuwa amemtimua meneja huyo.

 

Ukiweka hilo kando kidogo, tujikumbushe na tukufafanuliwe ilivyokuwa kiasi cha sakata hilo kufikia hapo. Moja ya sababu zaCannavaro kudaiwa kuwa chanzo cha kutimuliwa ni kutokana na kudaiwa kuwa alikutana na mwekezaji na bilionea wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, lakini baada ya uchunguzi wa uhakika wa gazeti hili imebainika kuwa wawili hao hawakukutana. Zahera alimtuhumu meneja huyo kwenda ofisini kwa Mo kwa ajili ya kuzungumza naye huku akitambua wazi timu hizo zina upinzani wa jadi na kuna ushindani mkali wa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

 

Gazeti la Championi limebaini kuwa Mo hayupo nchini kwa muda wa wiki mbili sasa, yupo nje kwa shughuli zake binafsi. “Zahera amepotoshwa na watu wake wa karibu wenye lengo la kumchafua Cannavaro na Mo, kiukweli siyo sawa na hizo taarifa alizozipata kocha siyo za ukweli.

 

“Kingine, ofisi ya Mo ipo ghorofani na haina mlango wa nyuma, sasa tunashangaa mlango upi wa nyuma alioutumia Cannavaro kuingia ndani kama ambavyo kocha alielezwa. “Hao watu wanaompelekea taarifa wanatakiwa kuwa makini, kwani kama ikiendelea hivi, basi ujue Zahera atajiweka pabaya, viongozi wa Yanga wanatakiwa kumtahadharisha kocha wao,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Baada ya maelezo hayo, tukirejea kwa Cannavaro, imeelezwa kuwa aliwasili mazoezini kwa usafiri wa gari la mtu wake wa karibu na kuendelea na shughuli zake za umeneja kama kawaida. Alipotafutwa Cannavaro mwenyewe juu ya kinachoendelea, alisema: “Mimi bado meneja wa Yanga niliyechaguliwa na viongozi. Hivyo sitatereka kwa lolote, nitaendelea kufanya kazi yangu ya umeneja kama kawaida, kwani nafasi hii ya uongozi hajanipa yeye (Zahera).”

Comments are closed.