CCM; Supu haiungwi nazi

CCMCHAMA Cha Mapinduzi (CCM) ni chama kikongwe, kimekomaa katika mambo ya siasa, kina uzoefu wa kutosha wa chaguzi tangu kilipoanzishwa 1977.

CCM hakina ugeni na ikulu kwa sababu kimekuwepo madarakani kihistoria zaidi ya miaka 50; uzoefu huu unatosha kuwafanya wanasiasa wake kuwa tofauti na wa vyama vya upinzani.

Ukomavu wa CCM kisiasa ndiyo uliolivusha taifa hili salama kwenye changuzi nyingi ukiwemo ule wa mwaka 1995 uliokuwa na mvutano mkali kati yake na chama cha NCCR-Mageuzi kilichowania kiti cha urais kupitia mgombea wake Augustino Mrema.

Ni CCM hii ndiyo iliyoshinda chaguzi zote na kuliacha taifa katika umoja na mshikamano, achilia mbali dosari kidogo ambazo zimekuwa zikijitokeza Visiwani Zanzibar ambako hata hivyo chachu yake imeshindwa kuchachua donge zima la kutoweka kwa amani.

Kwa namna yoyote chama hiki tawala kina historia tukufu ya uungwana na ujenzi wa taifa tulivu. Silaha hii imekivusha chama hiki miaka mingi kwenye chaguzi mbalimbali, hakuna wa kupinga.

Nakumbuka kwenye uchaguzi wa mwaka 1995; wananchi enzi hizo za uchanga wa mageuzi ya kidemokrasia waliambiwa, kuvichagua vyama vya upinzani ilikuwa ni hatua ya kukaribisha vita; hilo liliwaogofya watu wakakipa ushindi wa kishindo chama tawala.

Kauli za ‘hatukubali mpaka kieleweke’ hazikuwa sehemu ya utamaduni wa CCM; ilikuwa ni silaha ya vyama vya upinzani ambayo kwa miaka nenda-rudi imeshindwa kuwasaidia kupata madaraka.

Enzi hizo kauli mbiu za ‘jino kwa jino, mapanga shaa, ngunguri, ngangari’, zilimaanisha vyama vya upinzani ambavyo vilijengwa kwa misingi ya vurugu kama njia ya kuhalalisha upatikanaji wa kile kilichoaminiwa na vyama hivyo kuwa ni upataji wa haki.

Kwenye uchaguzi wa mwaka huu mambo yanaonekana kugeuka kidogo; kauli za ‘goli la mkono CCM si chama cha mchezo, lazima tutashinda, hatuko tayari kuiacha ikulu’, sasa zinatolewa na baadhi ya viongozi wa CCM.

Kipi kimekisibu chama hiki kikongwe mpaka kusahau mtaji wake wa kujizolea kura kwa misingi ya amani,  mimi sijui!

Lakini duru za siasa zinaonesha ni joto la uchaguzi wa mwaka huu linalopandishwa na presha ya mgombea urais Edward Lowassa ambaye amepewa nafasi ya kuviwakilisha vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ndilo linalowanyima usingizi CCM.

Napenda niwaambie baadhi ya viongozi wa CCM kuwa, supu haiungwi nazi; ukifanya hivyo unapoteza ladha yake na bila shaka hicho hakitakuwa chakula bali mchuzi unaopaswa kutowezwa na tonge.

Kauli ya mmoja wa makada wa CCM ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo, aliyoitoa hivi karibuni kwenye mikutano ya kampeni kuwa chama hicho hakiko tayari kuwaachia wapinzani ikulu, imekiharibia sifa chama hicho. Mimi naifananisha na nazi iliyogeuza supu kuwa mchuzi.

Kwa mtazamo wangu Bulembo hakupaswa kusema hivyo kwa sababu anayekabidhi ikulu kwa mtu siyo yeye wala chama chake bali ni wananchi. Akisema hawako tayari kuiacha ikulu anamaanisha shari.

Nawashauri viongozi wa chama hiki tawala kurudia misingi yake ya kuendesha siasa safi na kuacha kutoa kauli za kichochezi zitakazowajengea wananchi hisia kuwa CCM hakitatoka madarakani hata kikishindwa. Hisia hizi zitakuwa mwiba kwake pale kitakaposhinda kihalali.

Hakuna haja ya kuwaandaa wananchi katika hali ya kupinga matokeo wakati miaka yote tumefanya uchaguzi na mshindi alipatikana kwa amani.

Lazima tufahamu masilahi ya taifa ni muhimu sana kuliko chama kuingia au kusalia ikulu. Mara nyingi nimewaeleza wanasiasa hakuna faida kutawala watu wanaomwagana damu.

AMANI KWANZA MADARAKA BAADAYE!


Loading...

Toa comment