The House of Favourite Newspapers

CCM wamtimua Balozi Karume, urais watajwa

0
Balozi Ali Karume

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kusini Unguja kupitia kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM ya mkoa huo imeridhia kumfukuza uanachama Balozi Ali Karume kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wake pamoja na vitendo vya kada huyo ndani ya chama.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari  Julai 8,  2023 baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati ya ya Halmashauri Kuu ya CCM ya mkoa wa kusini Unguja Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM mkoa huo, Ali Timamu Haji amesema wajumbe wa kamati hiyo wamekubaliana kwa kauli moja ya kumvua uanachama.

“Hivyo Balozi Karume anatakiwa kurudisha kadi ya uanachama nambari C00/2809/9931 iliyotolewa Machi 17 mwaka 2022 na kadi ya zamani ni nambari CM/078856 iliyotolewa Februari 4 mwaka 2019,” amesema.

MBETO AMTOLEA UVIVU …

Aidha, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar, Khamis Mbetto Khamis amemtaka Balozi Karume kuheshimu katiba ya CCM, kanuni na taratibu zake.

Mbetto ameeleza hayo na kusema njia za ukosoaji anazotumia Balozi Karume zinakichafua chama hicho na si kukijenga.

Amesema matamshi yote yanayotamkwa na Balozi Karume laiti angeyatoa ndani ya vikao halali vya kikatiba isingekuwa kosa lakini kutamka kwake akiwa nje ya vikao ni hujuma na usaliti.

Pia, amesema kwa upeo, maarifa na uzoefu alionao kisiasa ni fedheha na aibu kwake kumsikia akikishambulia chama ambacho msingi wake umeasisiwa na mzazi wake aliyekuwa Rais wa ASP ambacho kiliungana na TANU mwaka 1977 na kuzaliwa kwa CCM.

“Si kweli kama CCM haina majibu ya kumjibu Balozi Karume, kinachelewa kufanya hivyo kwa kuwa nyumba anayokaa hivi sasa ndipo mahali alikoishi Hayati Rais wa kwanza wa Zanzibar,” amesema.

Amesema CCM hakisiti kumjibu Balozi huyo ila kinaona si adabu wala tabia njema kulitaja jina na kiongozi mkuu wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar au familia yake.

“Huwezi kuizungumzia ASP bila kulitaja jina Mzee Abeid Amani Karume, pia ni vigumu kuyataja Mapinduzi, Muungano hadi kuzaliwa CCM bila kuwahusisha waasisi wake akina Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Karume,” amesisitiza.

Amesema kama ilivyo ugumu wa kuizungumza TANU bila kukitaja TAA pia ngumu kuitaja ASP na kuiweka kando African Association hivyo CCM hakishindwi kujibu shutuma za Balozi Karume.

“Kwanini Balozi Karume atamke maneno haya sasa, alishindwa nini kukosoa wakati kaka yake Dk. Amani Karume akiwa Rais miaka 10 na kwamba kimejiri nini hivi siasa hata ainange serikali ya awamu ya nane?,” amehoji Mbetto.

Amesema ikiwa tatizo kutopata uteuzi wa kuwania urais, ajue kuwa Rais Dk. Mwinyi alipitishwa na vikao vya chama hivyo kumshutumu kila uchao ni kumkosea heshima kwani hata kaka yake alipokuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Balozi huyo hakuteuliwa.

“Balozi Karume asitazame mahali alikoangukia, atazame alipojikwaa ili aking’oe kisiki kilichomdondosha na kwamba anapomsakama kiongozi aliye na mamlaka ya juu kikatiba na kisheria lazima kwanza ajipime,” amesema.

Ikumbukwe Balozi Karume aliitwa na kuhojiwa na kamati za maadili za tawi la Mwera, jimbo la Tunguu na Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja kwa nyakati tofauti na kisha kupewa barua ya onyo.

Aidha, Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi alionekana kushangazwa na chama chake kushindwa kuwachukulia hatua makada wanaojitokeza hadharani na kukitukana chama.

Miongoni mwa kauli za Balozi Karume zilizosababisha kuitwa na kuonywa ni ya tuhuma dhidi ya chama hicho kuwa hakijawahi kushinda kihalali kisiwani humo na kumkosoa hadharani Rais Mwinyi kuhusu sera za kukodisha visiwa, akipinga utaratibu huo.

Pia alipinga utaratibu wa wananchi wa Kilimani kuondolewa, ili kujenga ukumbi wa kimataifa na ujenzi wa uwanja wa Amani akidai vinakiuka utaratibu.

Hata hivyo, licha ya kupewa barua ya onyo na kuwa chini ya uangalizi, hivi karibuni zimeonekana baadhi ya vipande vifupi vya video za mwanadiplomasia huyo akirejea kauli yake akisisitiza kwamba, licha ya kueleweka vibaya kwa chama chake, lakini hakuna demokrasia ya kweli ndani ya chama hicho.

“Ukijitokeza kuwania nafasi utasikia huyu sifa yake kubwa baba yake alikuwa Rais, huyu baba yake alikuwa Rais hakufanya vizuri, je, hiyo ndiyo sifa pekee? Na mmefanya uchunguzi kuona sifa zake nyingine?” alihoji.

KORUMBA wa GLOBAL TV ALIVYOMBANA MSEMAJI MKUU wa SERIKALI KUHUSU BANDARI na TOZO za SIMU…

Leave A Reply